WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia amempasha Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Hussein Mwinyi kuhusu ajira za madaktari akisema, wizara hiyo
ina utaratibu mbovu wa kuajiri unaowavunja moyo watumishi hao wa afya.
Ghasia na Mwinyi walitofautiana kuhusu suala hilo juzi kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kilichofanyika Dar es Salaam baada ya Dk Mwinyi kutoa taarifa ya wizara yake ambayo pamoja na mambo mengine, ilieleza kuwapo mmoja wa madaktari wastaafu aliyeajiriwa na kupewa cheo cha Mganga Mkuu wa Mkoa.
Katika taarifa yake zaidi, Dk Mwinyi alieleza kuwa kuna watumishi ambao hupata mishahara bila kufanya kazi mkoani Manyara na kwenye Chuo cha Mtapika, wakati pia kuna watoa huduma asilimia 50 waliopata mafunzo lakini hawazingatii viwango vya kukinga na kudhibiti maambukizi katika utoaji huduma za afya.
“Utunzaji wa dawa na vitendea kazi hauzingatii taratibu husika za uhifadhi na uhakiki wa ubora wa vipimo vya maabara, kuna uagizaji wa dawa nyingi kuliko mahitaji mkoani Mtwara, huduma zinazotolewa hazikidhi matarajio ya wateja katika vituo vingi vya afya,”alisema Dk. Mwinyi. Ghasia
Baada ya kumaliza kusoma taarifa hiyo mbele ya wajumbe wa kamati hiyo chini ya mwenyekiti wao Dk Faustine Ndungulile, Ghasia alisema baadhi ya matatizo kwenye wizara hiyo siyo ya msingi.
“Nina historia yake huyo daktari alishawahi kufanya mambo ya ajabu tu hadi yakaripotiwa kwenye vyombo vya habari sasa karudishwa na ndiye mganga mkuu, wakati nikiwa utumishi nililipata hilo na nikashauri aondolewe kwenye nafasi hiyo kwa kuwa hana sifa hiyo,” alisema.
Hatua hiyo ya Waziri, Ghasia ilitokana na taarifa aliyoiwasilisha Dk Mwinyi kwa kamati hiyo aliyoeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 wizara yake kupitia Idara ya Uhakiki na Ubora wa Huduma za Afya na Ustawi wa Jamii imefanikiwa kufanya ukaguzi katika idara, taasisi na vituo vya kutolea huduma vilivyopo chini ya wizara na kubaini kuna upungufu mkubwa wa kiutendaji.
Kauli ya Dk mtuhumiwa
Gazeti hili liliwasiliana na Mganga Mkuu huyo wa Mtwara, Saidun Kabuma ambaye alibainisha kwamba hana cha kuzungumza kuhusu hilo kwa sababu wizara ndiyo ilimpa nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment