Aliyekuwa
Makamu Mwenyekiti BAVICHA kabla ya kufukuzwa kwenye umoja huo mapema
mwezi huu, Bi Juliana Shonza (pichani) ameandika waraka mrefu akifafanua
kile alichokiita ni tamko lake kutoa ufafanuzi dhidi ya taarifa batili
zilizoelezea kufukuzwa kwake ambako kumepelekea pia kupoteza sifa za
uanachama wa CHADEMA kwa mujibu wa taarifa ya awali ya Mwenyekiti wa
baraza hilo Ndg John Heche. Ifuatayo ni tamko hilo la Juliana ambalo
limesheheni tuhuma mbali mbali, kashfa na maneno mengine yasiyofaa
kuzungumzwa na mtu anaedai bado ni kiongozi halali. Chukua muda usome
hii hapa chini….
TAMKO LA KUTOA UFAFANUZI DHIDI YA TAARIFA BATILI ZILIZOZALISHWA NA
MWENYEKITI
WA BAVICHA BWANA: JOHN HECHE [WEGESA CHARLES SUGUTA] KUHUSU KUVULIWA
UANACHAMA WA BAVICHA, NA KUSHABIKIWA NA MH. FREEMAN MBOWE, MWENYEKITI
CHADEMA TAIFA
Nawashukuru
sana wanahabari, kwa kuchukua muda wenu kuja kunisikiliza. Natambua
mnakiu ya kusikiliza mambo mengi ya kuwaeleza kutokana na taarifa
zilizosambaa kuhusu hiki kichefuchefu kinachosambazwa kwa makusudi na
virusi vichache vilivyojivika ngozi ya ukombozi.
Nimepokea
simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania
wakitaka kupata ufafanuzi baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya
habari kuwa nimevuliwa uanachama na U-Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA
Taifa.
Kama
mlivyo ninyi, nami pia nimeyasikia hayo kupitia vyombo vya habari, maana
sijapata barua au mawasiliano yoyote toka kwa Mwenyekiti wa BAVICHA,
Ndugu Wegesa Suguta (John Heche) aliyetoa tamko hilo.
Kwanza
kabisa naomba kuweka wazi kwamba sijawahi pewa shutuma zozote au
mashitaka yoyote yale yanayohusiana na hicho alichokiongea.
Niliamua
kupuuzia kwa sababu namjua Heche ni mlopokaji, kiongozi asiyejua wajibu
wake, anayetumikia wasiomchagua, mtu asiye na malengo na mtegemezi wa
siasa ili kuendesha maisha yake na ya familia yake.
Pia
nilimpuuza kwa sababu najua sio Mwenyekiti aliyechaguliwa kidemokrasia,
aliwekwa kwa matakwa ya wakubwa zake ambao wanamtumia kwa malengo
yaliyokusudiwa, ikumbukwe kuwa vijana watatu, Habibu Mchange, Mtela
Mwampambwa na Grayson Nyakarungu walienguliwa kimizengwe ili Heche
ashinde, hivyo kwetu sisi yeye ni sawa na Mwenyekiti wa kuteuliwa. Hivyo
sikumjibu mtu asiyekuwa na sifa sawa na zangu katika harakati za kusaka
demokrasia ya kweli.
Lakini
kitendo cha Mwenyekiti wangu, Mh. Freeman Mbowe kujitokeza kupitia
gazeti mojawapo na kudai madai yangu ni ya kitoto, kwanza
kimenifedhehesha, ni dharau kwa vijana walioniona nina sifa na ukomavu
na kunipa kura nyingi ili niwe Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa.
Pili
ni kama anahalalisha kikao batili, kilichokiuka kanuni na katiba ya
CHADEMA ili kuhalalisha matakwa yao yenye lengo la kuminya demokrasia na
uhuru wa kujieleza ndani ya chama.
Tatu
anahalalisha hoja za vijana, ambazo ndio uhalisia kuwa Heche hakuwa na
sifa, na uwezo, hivyo alibebwa na Mh. Mbowe ili akae pale kwa malengo
yake.
Ndio
maana nilisema ukiona kifaranga kimepanda juu ya figa ujue mama yake
yuko chini, hivyo mama yake kifaranga kajitokeza kuhalalisha kifaranga
chake kupanda juu ya figa.
MADAI YA ALIYODAI MH. MBOWE KUWA NI YA KITOTO
Niseme
wazi kwamba nimesikitishwa mno na madai aliyoyatoa Mwenyekiti wangu wa
CHADEMA Mh Freeman Mbowe kupitia gazeti la Mtanzamia la tarehe
12/01/2013 kwamba madai yangu ni ya kitoto .
Kwanza
niweke wazi kabisa kwamba namuheshimu sana Kiongozi wangu huyu mkuu
ambaye ndiye alipaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba
haligawi baraza la Vijana na chama kwa ujumla, ahakikishe kuna utawala
bora ndani ya chama, na utendaji haki, lakini cha kushangaza ameibuka
kumtetea Heche kwa hoja za mwegemeo wa upande mmoja bila kuangalia
maelezo ya upande wa pili.
Niweke
wazi kabisa kwamba kauli aliyoitoa dhidi yangu ni yakiushabiki maana
kama ni madai yangu kuhusu namna ninavyohujumiwa kupitia kwa Katibu Mkuu
yeye anayo nakala ya malalamiko [ushahidi upo], lakini hakuna hatua
ambayo ameichukua.
Namshangaa
Mwenyekiti kudai madai yangu ni ya kitoto sasa sijui ni madai yapi
anayazungumzia ? madai ya kitoto ni yapi? na madai ya kikubwa ni yapi ?
na je madai ya kitoto ni haya mimi kuhoji kwanini hatuweki akiba kwenye
akaunti kwa ajili ya uchaguzi 2015 kama tulivyokubaliana kwenye baraza
kuu mara baada ya uchaguzi wa 2010.
Naomba niwajulishe wanachadema kuwa, nimejitahidi sana kushauri juu ya
1;
Uanzishwaji wa chuo cha mafunzo ya uongozi kwa makada wa CHADEMA ,
badala yake ni matumizi mabaya ya fedha za ufadhili wa wadau tofauti na
hasa mfadhili mkuu ndugu SABODO. Hii ingesaidia pia kulea ki-mfumo wa
maadili ya uongozi kwa vijana wa umoja wa wanafunzi wa CHADEMA wa vyuo
vikuu yani “ CHASO” ambapo mimi ni mwasisi wa mkakati huu nchini.
2;
Chama kwa ujumla kutokuwa na jengo letu na hasa makao makuu yetu. Ni
aibu kwa chama kikubwa kama CHADEMA kuwa na ofisi tulizopanga na kulipa
mamilioni ya fedha za ruzuku na misaada kwa manufaa ya Mwenyekiti
Freeman Mbowe na Mkurugenzi wa fedha wanaomjua mmiliki wa jengo la makao
makuu. Kimsingi mimi natambua chama kina uwezo mkubwa wa kuwa na
majengo yetu.
3;
kupunguza mshahara wa katibu mkuu Ndugu Dk. Slaa ambao ni zaidi ya
milioni saba kwa mwezi na marupurupu kibao ili pesa hizo na mamilioni
zielekezwe kujenga chama mikoani kama kweli tunataka 2015 tuingie Ikulu.
4;
kuhakikisha pesa zilizochangishwa kwenye M4C zinatumika ipasavyo na si
kama zitumikavyo kipindi hiki ambapo ni kama tumelewa wingi wa watu
kwenye mikutano ya hadhara.
5;
Kitendo cha Mwenyekiti wa chama kufumbia macho hatua ya ndugu
Slaa-katibu mkuu kujikopesha pesa ya ruzuku ya watanzania zaidi ya
shilingi milioni mia na arobaini.
7;
Hatua ya mwenyekiti ndugu Heche kulipwa mshahara na marupurupu hali
kanuni za chama haziruhusu huku Mbowe akifumbia macho wakati viongozi wa
mikoa na wilaya hawapewi pesa na vifaa vya uenezi.
8;
kitendo cha mchumba wa Dk. Slaa,; Josephine Mushumbushi kuzunguka
mikoani na kulazimisha kupokelewa kama mke wa mfalme na kuendesha vikao
vya ndani na mikutano ya hadhara yenye kulenga kuwajenga wagombea ubunge
anaowataka yey e na katibu mkuu kwa mwaka 2015.
Ndugu
wanahabari, je hizi ndo hoja za kitoto anazodai Mh. Mbowe? Hivyo basi
namtaka Mh. Mbowe sasa asikimbilie kujibu hoja kiushabiki. Ajitahidi
kuwa na fikra na Busara ili kukisaidia chama kuvuka kwenye daraja la
sasa la pepo kufukuzana. Atambue Baraka anazozitoa wanachama wafukuzwe
hovyo na kunyanyaswa ni hatari kwa kuwa anaandaa kundi kubwa nje ambalo
litageuka mwiba siku za usoni.
UHALISIA ULIOPO
Ndugu
waandishi wa habari, Naomba kuweka wazi kwamba mimi Juliana Shonza ni
Makamu Mwenyekiti halali wa baraza la vijana (BAVICHA). Taarifa zozote
zile mlizozisikia kuhusu kuvuliwa kwangu uanachama, naomba kwa nguvu
moja kupitia taaluma yenu muwaambie watanzania kwamba wazipuuze. Ni
taarifa zilizotolewa na kikundi cha kihuni kilicho lenga kutimiza
matakwa ya wakubwa wao. Kikundi hicho hakina mamlaka ya kikatiba yoyote
yale ya kunivua uongozi huu nilio nao.
Kuthibitisha
hilo kuwa ni kikundi mufilisi, hadi ninapoandika waraka huu kwenu
sijapewa barua yoyote ile inayonitaarifu kuwa nimevuliwa uongozi wangu.
Hii ni wazi wanatambua kuwa wanachemka, wanatengeneza makundi kwa
maslahi wanayoyaona yanawafaa.
Sikuchaguliwa
ili niwe chombo cha kuwatumikia watu, na badala yake nilichaguliwa ili
niwatumikie vijana wa CHADEMA na watanzania kwa ujumla, na pale
nilipoona kuna ukiukwaji na kuhoji ndio chanzo cha mizengwe na matamko
ya Ndugu Wegesa (John Heche).
Nimekuwa
nikiwasumbua viongozi wenzangu kuhusu kutengeneza kadi za BAVICHA na
kusajili wanachama katika mfumo mzuri (database) ili tuwe na kumbukumbu
ya wanachama wetu lakini yote yameshindikana kwa sababu amekuwa
akiendeshwa na mfumo dume kandamizi kwa mwanamke, mara nyingi
nimemshauri kwa ajili ya maendeleo ya Baraza na nimekuwa nakwamishwa na
Mwenyekiti na Katibu na hata leo sisi wote ni wanachama kwa kufikirika
(imagination), kwa kuwa bado hatuna kadi za uanachama kwa vijana wa
BAVICHA zaidi ya kutambulika na katiba ya chama.
KUKIUKWA KWA KATIBA
Ndugu
wanahabari, ni wazi kuwa katiba pamoja na mwongozo wa baraza letu la
vijana bavicha ulikiukwa katika kikao walichokiita kamati tendaji
iliyokaa tarehe 05/01/2012 ambayo iliongozwa na Bwana Wegesa Suguta
(John Heche) kama Mwenyekiti, hali inayonilazimu kusema wazi, bila
kumung’unya maneno kwamba maamuzi yaliyotolewa na kikao hicho yalikwisha
pangwa na viongozi wa kitaifa hayakuwa halali.
Nasisitiza
kwamba ni ukweli ulio wazi kwamba agenda na maazimio ya kikao hicho
yalikwisha amuliwa hata kabla ya kikao hicho kwasababu kubwa mbili
1;Taarifa
za kufukuzwa kwetu zilikwisha anza kusikika kwenye mitandao ya kijamii
kama vile jamii forum na facebook mwezi mmoja kabla ya kikao cha kamati
tendaji batili.
2;Pili
ushahidi wa kimazingira kwa maana ya ukiukwaji mkubwa wa kikatiba na
mwongozo wa Baraza letu la Vijana uliofanyika siku ya kikao.
Ndugu
wanahabari ikumbukwe kuwa pamoja na uwepo wa taarifa za kikao mwezi
mmoja kabla binafsi nililetewa taarifa hizo siku mbili kabla ya kikao,
tena kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi {sms} na baadae kupigiwa simu
na Katibu wa Baraza Bwana Munishi ikinitaka kuhudhuria kikao hicho
kutokana na kuwa nje ya Dar-es –salaam kwa mambo yakifamilia zaidi
niliwataarifu viongozi wenzangu kwa utaratibu maalumu wa mawasiliano ya
kiuongozi kwa maana ya kuwatumia barua ya udhuru wakutohudhuria kikao.
Lakini
chakushangaza na kustaajabisha kwa viongozi wenzangu hawa ambao kwa
namna moja ama nyingine napata ugumu wakuelewa kama kweli wana sifa za
kuitwa viongozi tena wa idara nyeti sana katika ustawi wa chama chetu
,kwa makusudi kabisa ama kwakutumwa kufanya hivyo ama kwa utashi wao
mdogo wa kiupembuzi yakinifu waliamua kuvunja na kukiuka katiba ya chama
na kujipa vyeo vya kiunyampara kwakuamua kuchukua maamuzi yakutuvua
uanachama wa kufikirika wa baraza mimi na vijana wenzangu Ndugu
Mwampamba na Mchange ambao nao hawakupewa nafasi yakusikilizwa, ambao
moja kwa moja tunapoteza sifa yakuwa wanachama wa CHADEMA.
Ndugu
wanahabari naomba sasa nijikite katika katiba ya chama changu na
mwongozo wa baraza la vijana sura ya sita kipengele cha 6.5 ambacho
kinasema taratibu zifuatazo lazima zifuatwe katika kuchukua hatua za
kinidhamu. 6.5.2 kwa mujibu wa ibara 5.4.3 na .4.4 ya katiba, mwanachama
yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama
kufukuzwa uanachama bila kwanza
{a} kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.
[b] kupewa nafasi yakujitetea katika kikao kinachohusika.
{c} Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao mnamo wiki mbili baada ya kusikilizwa.
Ndugu
waandishi wa habari,Niseme wazi kwamba hakuna kifungu kilichofatwa kati
ya hivyo niliyoviainisha hapo juu, hakuna barua yeyote niliyojulishwa
ya hayo waliyoyaita mashitaka yangu zaidi yakuyasoma na kuyasikia kwenye
vyombo vya habari baada ya wao na kikao chao haramu kuchukua maamuzi
yakunivua uanachama wa Bavicha .
Sikupewa
nafasi yakujitetea maana sikuwepo kwenye kikao, barua ya udhuru
wakutohudhuria walikuwa nayo. Na vile vile mpaka leo hii sijajulishwa
kwa maandishi uamuzi wa kikao hicho batili badaa yake viongozi wenzangu
hawa wameamua kuujulisha umma wa Watanzania na wanachadema kwa ujumla
pasipo kunijulisha mimi kwanza.
Ukiangalia
pia kifungu cha 6.5.6 cha katiba kinasema KIONGOZI YEYOTE hatachukuliwa
hatua za kinidhamu bila kwanza kupewa mashitaka kwa maandishi na
mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu kwa maandishi. Sasa basi
namtaka Bwana Wegesa Suguta awaeleze umma wa watanzania kama
alivyokurupuka kuwaeleza kwamba Shonza amevuliwa uanachama wa Chadema ni
wapi na lini yeye kama Mwenyekiti nilipewa barua ya hayo wanayoyaita
mashitaka, na ni lini niliwapa majibu ya mashitaka hayo.
UHALALI WA KIKAO CHA KAMATI TENDAJI
Ndugu
wanahabari ikumbukwe kwamba kikao cha juu kuliko vyote kwenye ngazi ya
chama husika ni Mkutano Mkuu ambao ndio ulioniweka madarakani kutokana
na kuwa na imani na mimi na kikatiba ndio haswa ulipaswa kuniandikia
mashitaka, kunijadili, kunihoji na kutoa maazimio ambayo yangepelekwa
kamati kuu ambao kimsingi ndiyo yenye mamlaka ya mwisho yakumvua mtu
yeyote uanachama wake baada ya kujiridhisha na taarifa na uchunguzi
kutoka kwenye kikao husika kilichomwandikia mwanachama mashitaka na
kumuhoji.
Ndugu
wanahabari ifahamike wazi kwamba kikatiba kuna ngazi mbili tu
zinazoweza kumvua mtu uanachama wake ambazo ni ngazi ya tawi na ngazi ya
kamati kuu. Hivyo basi namtaka sasa Bwana Wegesa Suguta auambie umma wa
watanzania kwamba ni lini kamati tendaji ya vijana iligeuka ama
kukaimishwa madaraka ya ngazi ya tawi, ngazi ya mkutano mkuu ama kamati
kuu yakuwa na uwezo wakumvua kiongozi uanachama wake?
Ndugu
waandishi wa habari, Wajumbe wa kamati tendaji kikatiba ni makatibu wa
kamati za uratibu za mikoa lakini badala yake Bwana Wegesa Suguta (John
Heche) amekuwa akiwaita wenyeviti wa mikoa na sababu kubwa ikiwa ni
kwamba wengi wa wenyeviti hao hawastahiri kuwepo bavicha kutokana na
kwaba umri wao kuwa zaidi ya miaka 35 hivyo kupoteza sifa zakuwa
viongozi wa bavicha ambayo katiba inamtaka mwanabavicha yeyote kuwa na
miaka 18-35, hivyo basi kwakuhofia kupoteza nafasi zao hulazimika
kukubaliana na lolote lile ambalo bwana Wegesa Suguta analitaka hata
kama wakijua kwamba ni kinyume kabisa na matakwa ya katiba na mwongozo
wa baraza. Hivyo kumpa Heche mwanya wakuamua lolote lile analotaka ama
kutumwa kulifanya.
Kutokana
na hilo natangaza wazi kwamba kikao cha kamati tendaji kilichopita ni
batili, chenye wajumbe batili, kimesimamiwa na viongozi batili kwa maana
ya mwenyekiti na katibu wake maana wameshindwa kuheshimu misingi ya
kikatiba katika namna ya demokrasia ya chama chetu hivyo basi nachukua
nafasi hii kuutangazia umma wa watanzania na wanachadema kwa ujumla wao
kwamba maamuzi ya kamati tendaji yaliyotangazwa na kiongozi kilaza na
daraja la viongozi wa juu bwana Wegesa Suguta ni batili.
Ndugu
wana habari, sifa ya Mwalimu ni kuweza kubadilisha hali ya umbumbumbu
wa wanafunzi wake, Heche kama kiongozi, na Mwalimu kitaaluma (nina
wasiwasi na ufaulu wake katika huo ualimu) alipaswa kuwa mfano bora kwa
vijana wa Chadema kuwaelekeza na kuwafundisha namna yakuheshimu misingi
ya kikatiba ambayo kama chama na baraza tumejiwekea na tunapaswa
kuifuata ni wazi kuwa Heche ameshindwa kuwa mfano bora kwa vijana, hajui
kanuni za BAVICHA wala katiba ya CHADEMA, mkurupukaji, mropokaji,
mwenye uwezo mdogo wa kufikiri, dikteta anayetumia mamlaka asiyokuwa
nayo (akipewa mamlaka atatuchinja huyu) hivyo hafai kuwa hata Mwenyekiti
wa serikali za mtaa, wala kuaminiwa popote kupewa nafasi ya kiuongozi.
Ni wazi ubongo wake yeye na katibu baraza bwana Munishi haujapewa tohara
la kisiasa, ifike mahali wakubali kufundwa unyagoni na manyakanga wa
kisiasa.
KUHUSU KUVULIWA UANACHAMA WA BAVICHA;
Ndugu
wanahabari, kuhusu kuvuliwa uanachama wa Bavicha ambao moja kwa moja
napoteza sifa ya kuwa mwanachadema namshangaa kiongozi huyu ambaye sifa
yake kuu siku zote ni ukurupukaji kwakusema kwamba nimevuliwa uanachama
wa Bavicha huku akijua wazi Bavicha haijawahi kuwa na kadi za baraza.
Katika mwongozo wa baraza la vijana kipengele cha 4.4 KUJIANDIKISHA UANACHAMA
4.4.1 inasema ili kijana aruhusiwe kujiunga bavicha ni lazima awe na sifa zifuatazo
[a] Awe mwanachama wa CHADEMA
[b] Awe na umri kati ya miaka 18 na 35
[c] Awe anakubaliana na misingi ya mwongozo wa BAVICHA
4.4.2 Inasema kijana aliyekidhi matakwa hayo hapo juu, atanunua kadi ya uanachama wa BAVICHA
Kutokana
na kipengele hicho namtaka bwana Wegesa Suguta auambie umma wa
watanzania na wanachadema kadi yake yeye ya baraza la vijana ni namba
ngapi na aliichukulia wapi? Aueleze umma wa watanzania kadi yangu ya
baraza la vijana ni namba ngapi na niliichukulia wapi?
Ndugu
waandishi wa habari,Ni dhahiri baraza la vijana chadema hatuna kadi
ambayo kimsingi ndiyo utambulisho wa mwana bavicha endapo akishakidhi
sifa zilizoainishwa hapo juu. Na ni wazi kwamba vijana wote wa chadema
tuna sifa za kuwa wana Bavicha lakini si wanachama wa BAVICHA kutokana
na kwamba nimekuwa nikimwambia mara kwa mara umuhimu wa kuirasimisha na
kuianzisha ili iwe taasisi kamili kwa kuwa na kadi za vijana kama
mwongozo wa vijana unavyojieleza.
UELEWA WANGU KUHUSU KUNDI ANALOLIITA NDUGU WEGESA SUGUTA (JOHN HECHE) NI “MASALIA”
Ndugu
waandishi wa habari, Hakuna kundi linaloitwa masalia ndani ya Chadema
na BAVICHA. Gazeti la MWANAHALISI ndilo lililoandika kuwa vijana wote
waliofutwa na kuondolewa kwenye uchaguzi wa BAVICHA mwaka 2011 ni
MASALIA ya Zitto yanayopukutishwa Chadema. Kimsingi gazeti hili lilikuwa
linafanya kazi yake ya kipropaganda ndani ya CHADEMA ili kukigawa
Chama. Lilikuwa linatimiza wajibu wake wa kupika mpasuko ndani ya chama
tena kwa kuhusisha na viongozi wakubwa ndani ya chadema.
Ni
aibu kubwa sana na ni hatari kuona kiongozi kama Wegesa Suguta anakuwa
mstari wa mbele kushabikia neno masalia, huku akijua wazi kufanya hivyo
ni kuligawa baraza la vijana. Kwa nguvu moja nalaani kitendo hiki cha
kipuuzi kinachofanywa na Mwenyekiti huyu wa BAVICHA cha kuchekelea
upuuzi uliopikwa na gazeti la Mwanahalisi.
Naomba
atumie rasilimali za chama kujenga umoja wa vijana imara, tushirikiane
kuimarisha Bavicha yenye tija kwa chama na sio kusherekea mpasuko ndani
ya baraza la vijana.
UELEWA WANGU KUHUSU KITU KINACHOITWA PM7
Ndugu
waandishi wa habari, Naomba kunukuu maneno ya mtu maarufu sana
mitandaoni na kwenye uga wa habari Mzee mwanakijiji anasema”Uongozi
imara sio kutegeana, kunyemeleana na kufukuzana. Uongozi imara ni
kushirikiana”.PM7 ni jina lenye maana ya “PATRIOTIC MOVEMENT” yaani
harakati za kizalendo kwa mujibu wa Ndugu Ben saanane ambaye alitumwa na
kiongozi wa juu wa chama kuja kulitekeleza kwa vijana walioenguliwa
kwenye uchaguzi wa BAVICHA mwaka 2011 na wanaoonekana kusigana na
kiongozi huyo kimawazo. PM7 ni wazo liliobuniwa na kiongozi mmoja wa juu
wa chama akishirikiana na Ben saanane wakinuia kutega mtego wa kuwanasa
vijana wanaoonekana wapo tofauti kimawazo na kiongozi huyo wa chama.
Kwa
kuwa wazo hilo lilikuwa halina manufaa kwa chama, halikutekelezwa.
Kiongozi huyo bila kumung’unya maneno ameamua kuwa tumia vijana hao
kuandaa kikao batili cha kamati tendaji ya John heche ili awafukuze
vijana hao. Hii ni hatari sana kuona kiongozi wa chama unageuka simba na
kuanza kuwawinda watoto wake ili uwamalize kisiasa kwa sababu zako
binafsi.
MAAJABU KATIKA MEDANI ZA SIASA ZA BAVICHA MWAKA 2013
Ndugu waandishi wa habari.
1.
Hii ni ajabu sana katika kikao cha kamati tendaji batili, Ambao
hatukuhojiwa ni watu wawili, mimi Juliana Shonza na kijana mmoja anaitwa
Exaud Mamuya. Lakini Mimi Juliana Shonza nimehukumiwa bila hata
kusikilizwa wala kupewa mashitaka na chombo chochote katika chama.
Wakati huo huo Exaud Mamuya hajahukumiwa kwa madai hakufika kwenye kikao.
Hii ni dhahiri huu ni mkakati wa kipuuzi ambao unaendeshwa na watu wapuuzi tena kwa misingi ya kikabila na kikanda.
2.
Muasisi mwenza wa PM7 na kibaraka wa kiongozi wa juu wa chama
aliyetumika kutoa shutuma chafu kwa Naibu Katibu Mkuu. Kijana
anayefahamika kwa jina la Ben Saanane ameachwa kwa madai yeye amekiri
mbele ya hiyo kamati tendaji kwamba ni kweli alinuia kumchafua Naibu
Katibu Mkuu wa chama na kukivuruga chama. Wakati tuhuma zake zinafanana
na za Mchange na Mwampamba.
3.
Mkakati wa John heche na vibaraka wake umejikita kutukuza ukanda ndani
ya chama tena wa wazi wazi. Ukanda huu umejidhihirisha kwenye kutoa
hukumu batili za tuhuma kama ifuatavyo.
-Vijana
waliohukumiwa wote ni wale wanaotokea Mbeya, Mbozi na Kibaha. Wakati
-Vijana wa Kilimanjaro wameachwa kwa madai wao wametoa ushirikiano.
Waliohukumiwa ni:
_Mtela mwampamba-Mbozi, mbeya
_Habib Mchange-Kibaha, pwani
_Juliana Shonza-Mbozi, mbeya
- Joseph kasambala – mbeya mjini (kasimamishwa)
- GWAKISA Mwakasendo –Rungwe, mbeya (kasimamishwa)
Pamoja na wanachama watatu waliopo mbeya mjini waliofukuzwa uanachama.
Waliosamehewa ni:
_Ben saanane-Kilimanjaro
_Exaud Mamuya-Kilimanjaro.
Hii
ni dhamira ya wazi kabisa kwamba CHADEMA sasa ni chama cha kikanda,
Viongozi wa chadema wanatumika kutangaza ukanda kwa watanzania. Kwa
maana hiyo wale wote wasio wakaskazini ndani ya Chadema tusitegemee
kutendewa haki.
MAMBO NILIYOMSHAURI HECHE NA KUMUONYA
Ndugu
waandishi wa habari, Sisi kama vijana tusigeuze siasa kuwa ajira wala
chombo cha kuendeshea maisha, ni moja ya vikwazo katika kukuza
demokrasia ya kweli, maana wengi wanaendekeza njaa na uhitaji wa maisha
yao ili kupindisha ukweli.
Moja
ya maswali yangu kwa Mwenyekiti ni kitendo cha kubinafsisha gari
alilotoa Naibu Katibu Mkuu kwa ajili ya BAVICHA na badala yake
akalifisadi, akafanya mali yake binafsi na kumuweka Mdogo wake Chacha
Heche kuwa dereva wake, nimekuwa nikipinga matumizi mabaya ya rasilimali
hiyo kwa manufaa binafsi, na badala yake gari hiyo ifanye kazi
iliyokusudiwa, huu ni msingi wa kuonyesha tofauti yetu na wanaotumia
rasilimali za serikali (Taifa) kwa manufaa binafsi nay a familia zao.
Pia
nilimshauri Mwenyekiti awe na kipato halali kama katiba ya chama
inavyosema Sura 10 MAADILI YA VIONGOZI ibara ya 10 kifungu cha (6)
kinasema Kiongozi anatarijiwa kujitosheleza yeye na familia yake kwa
mapato halali ili kutokuwa ombaomba kwani tabia hiyo itadhoofisha uwezo
wake wa kutoa uamuzi sahihi, ili kuwa mfano bora wa uwajibikaji kwa
vijana, kama ambavyo Mwalimu Nyerere alivyosema kipimo cha Utu ni
kufanya kazi, badala yake ametelekeza taaluma ya ualimu, aliyotumia pesa
za walipa kodi kwa kusoma na muda wote ni kupiga soga bila uzalishaji
na kujipatia kipato halali, na badala yake anategemea mshahara usio
halali kuishi, ni wazi Mwenyekiti ni cheo cha kisiasa na hatakiwi
kulipwa mshahara, wala kulipiwa nyumba kwa mujibu wa kanuni. Badala yake
majibu anafikiri ni kufanya njama na waliopindisha taratibu hizo ili
alipwe mshahara kwa maslahi yao ya kisiasa. Na tumekuwa tukilipinga hilo
kwani tunataka tuwe mfano wa utawala bora kwa vitendo na si maneno peke
yake.
MWISHO:
Ndugu
waandishi wa habari,Nipo kwenye mchakato na wanasheria wangu
kushughurikia swala la kumpeleka mahakani Bwana John heche na gazeti la
Tanzania daima toleo namba 2958 kwa kuniita msaliti wa chadema, natumiwa
na CCM na kuwa nina mahusiano (natumiwa)na Wassira tena bila kunihoji
mimi Juliana Shonza. Kwa maana hiyo wamenichafua na kunidhalilisha mbele
ya umma wa watanzania.
Pili
naomba kuweka wazi kwamba natarajia kuomba ufafanuzi wa kikatiba juu ya
shutuma zilizotolewa kwenye vyombo vya habari dhidi yangu na bwana
Wegesa Suguta (John heche) ili aseme ni aminisho lipi la kuthaminisha na
kusakidikisha mtazamo wa maono yake ili bongo za watanzania zijue
ukweli.
Mimi
Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA natangaza rasmi Mtela Mwampamba na Habib
Mchange ni wanachama hai na halali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA). Hivyo nawaomba waendelee na kazi zao za ujenzi wa chama
kwenye majimbo yao na taifa kwa ujumla. Nawaomba wananchi na wanachama
wote wa chadema waendelee kuwa na imani dhidi ya vijana hawa. Kama
mlivyomwamini Mwampamba na kumpa kura 32000 na kama mlivyo mwamini
Mchange na kumpa kura 10400 kwenye uchaguzi wa Ubunge mwaka 2010. Vivyo
hivyo naowaomba muendelee kushirikiana nao kuhakikisha wanatimiza adhima
ya ukombozi mwaka 2015.
Wenu katika ujenzi wa demokrasia makini
Juliana Daniel Shonza
No comments:
Post a Comment