TUMSHUKURU Mungu kwa yote ambayo sisi tunayaona na mengine yaliyo juu
ya upeo wa macho yetu. Mzingo wa maisha umejaa changamoto nyingi,
Mwenyenzi anatulinda kila nukta, lakini hata kama hujui hilo, basi pumzi
ya uhai ikupe sababu ya kuamini kudura za Maulana.
Kwa uwezo niliojaliwa na Mola Mpaji, leo nachambua mada inayohusu
makundi ya wanawake na mitazamo juu ya wanaume. Ninachozingatia hapa ni
fikra katika makundi ambayo nayachambua hapa, vigezo vyao kwa wanaume
vipo kimtazamo zaidi.
Fikra
zao ndizo zimetengeneza mtazamo kwa namna ambayo wao wamepima maslahi
yao kwa wanaume. Maisha yanavyosogea mbele ndivyo binadamu wanavyojihisi
wana akili na maarifa zaidi. Sasa wanajiona wana uwanja mpana zaidi wa
kuchanganua, kuchambua na kuchagua.
Wakati miaka ya nyuma kila mwanamke ndoto yake kuu ilikuwa kuolewa
ili apate mume wa kutulia naye, hivi sasa mambo yamebadilika. Makundi ni
mengi, hata hilo ambalo linaundwa na wale wanaoteswa na kupata waume
lipo lakini halitambi, linabezwa.
Sababu ya kundi hilo kubezwa ni mtazamo uliopo kwenye makundi mengine
mawili kuwa watu wanaoota kupata wanaume wa kuwaoa, mawazo yao ni ya
kale. Kwamba hayajitoshelezi kwa kizazi cha sasa ambacho kimeegemea
teknolojia na utandawazi.
Tamaa ya fedha na kupanuka kwa sanaa, video zinazowaonesha mastaa wa
Marekani na Ulaya pamoja na mitindo yao ya maisha, kumechangia kwa kiasi
kikubwa kuwafanya baadhi ya wanawake kutengeneza mitazamo yao ya
kupenda.
KUNDI LA KWANZA
Mara nyingi linaundwa na wasichana wadogo na hata wanawake wakubwa
wenye fikra ambazo ni rahisi kuziita changa. Hawa hupenda wanaume
kutokana na muonekano wao. Inawezekana ikawa ni mtindo wa mavazi au
umbile lake.
Katika kundi hili, ni rahisi kukuta mwanamke ameangukia kwa mwanaume
asiye na malengo yoyote ya maisha. Matokeo yake, mwanamke huyo ndiye
anageuka mlezi wa mwanaume husika, akimhudumia kila kitu.
Mathalan, anavutiwa na urefu, atafanya juu chini mpaka ahakikishe
amemtia kwenye himaya yake. Hata kama hana ujasiri wa kusimama mbele ya
mwanaume na kuwasilisha hisia za moyo wake lakini namna atakavyokuwa
anaonesha kupagawa, itatosha kufikisha ujumbe.
Inawezekana pia ikawa kwa umbo lake lililojengeka kimazoezi. Ipo
mifano ya mabaunsa wengi tu mjini ambao kimuonekano tu, ipo wazi kuwa
wana nguvu za kutosha ambazo wangezitumia katika shughuli mbalimbali za
uzalishaji mali. Ajabu ni kuwa misuli na nguvu zao havina faida, kwani
wanalelewa tu na wanawake.
Hata mavazi, jinsi mwanaume anavyobadili mavazi, inaweza
kumsababishia mwanamke kuingia kichwakichwa. Sura nayo ni kielelezo
pamoja na sifa nyingine ambazo huonekana wazi katika mwili wa binadamu.
Ongezea rangi, mpangilio wa meno, anaweza kupenda mwanya tu!
Yupo mwanamke ambaye anaweza kudondoka kwenye penzi kwa sababu mwanaume mwenyewe huwa anavaa miwani.
Itaendelea wiki ijayo.
Chanzo cha hii ni Global Publishers
No comments:
Post a Comment