NDUGU zangu, kuna ambao wapo katika uhusiano lakini hawajui mambo ya
kufanya ili wawe bora kwa wapenzi wao. Mada hii itagusia pande mbili.
Upande wa kwanza ni kwa wale ambao ndiyo kwanza wapo katika hatua za
mwanzo kabisa na wapenzi wao na upande wa pili ni kwa wale ambao tayari
wapo katika uhusiano lakini hawajui jinsi ya kuwafanya wawe bora kwa
wapenzi wao.
Inawezekana wewe ukawa mmoja wao, sasa huna sababu ya kukata tamaa na
kuona kuwa huna thamani tena kwa mpenzi wako. Kwa kufuatilia vyema
vipengele vifuatavyo, naamini kwa namna moja au nyingine utakuwa mpya na
penzi lako litazidi kudumu zaidi na zaidi.
MWANZO WA PENZI
Siku zote nimekuwa nikisisitiza kuwa, jinsi unavyoanza ndivyo
utakavyomaliza! Kama ulianza vibaya uhusiano wako tegemea kumaliza
vibaya.
Kama unatarajia kuingia katika uhusiano na mpenzi mpya
hakikisha hujioneshi tofauti na hali yako halisi ilivyo! Jifunze
kujikubali, hata kama unafanya kazi ambayo unadhani ni ya hadhi ya
chini, mweleze mpenzi wako hali halisi ilivyo. Kama anakupenda, kazi
yako haiwezi kupunguza mapenzi baina yenu.
Ikiwa ndiyo kwanza mnaanza
uhusiano, zingatia hili na kama mpo katika uhusiano kwa muda mrefu
ukagundua wazi kuwa kuna mahali ulikosea, anza kufanya mabadiliko
kuanzia sasa. Bado hujachelewa, mwambie ukweli naye atakuheshimu
kutokana na ukweli wako.
Kudanganya hakuna mantiki, kudanganya ni
utumwa, usikubali kuingia katika utumwa au kifungo cha aina hiyo. Ukweli
ni silaha ya kwanza katika mapenzi, anza hivyo kuanzia mwanzo na kama
ulikosea, ulijisahau au hukujua, basi anza leo!
JIPENDE, JITHAMINI
Itakuwa kichekesho kama utasema unampenda mpenzi wako wakati wewe
mwenyewe hujipendi! Huwezi ukasema unamthamini mpenzi wako wakati
thamani yako mwenyewe huitambui.
Hivi kama unashindwa hata kuoga na
kubadilisha nguo safi nani atakayekupenda? Huwezi kuwa wa kisasa kama
huzingatii usafi, hakuna atakayevutiwa na wewe kama wewe hutaki
kujivutisha. Sio ajabu mpenzi wako akakutosa kwa sababu tu huna
muonekanano mzuri kwa rafiki zake.
Nani atakayekupenda wakati wewe
mwenyewe huonyeshi kama unajitambua?
Jikubali, jithamini! Kuwa msafi
wakati wote, kauli zako ziwe safi siku zote mpenzi wako atakuwa huru
kuwa na wewe. Isifikie hatua mpenzi wako akataka kutoka na wewe lakini
akasita kwa sababu hajui ukija utakuwa umevaa nguo za namna gani. Upo
hapo?
MWONEKANO WAKO
Mwonekano wako unaweza kukuainisha jinsi ulivyo kwa wanaokutazama,
wakati mwingine inawezekana ukatafsirika tofauti na ulivyo kutokana na
jinsi unavyovaa na tabia zako nyingine.
Lazima uwe kijana wa kisasa,
kwa kuzingatia hilo unapaswa kuwa makini kwa kila kitu kinachoonekana
kwa wanaokutazama. Jenga mazoea ya kutambua aina ya nguo na mahali
ulipo, usivae nguo za ufukweni ofisini au nguo za mtaani ukavaa
ofisini.
Wanaokuangalia wanapata taswira ya jinsi usivyo makini kutokana
na mavazi yako. Vaa nguo safi kila wakati labda kama unafanya kazi
ambayo inakulazimu kuwa mchafu, ila baada ya hapo unapaswa kuwa msafi.
Ukizingatia hili utamfanya mpenzi wako afurahie kuwa na wewe siku zote.
Amini popote ulipo, jinsi ulivyo ndivyo anavyoonekana mpenzi wako.
Kutokana na nafasi yetu, hayo kwa leo yanatosha, nitakuwa nikizidi kukupa yale yanayoweza kukufanya uwe bora kwenye uhusiano wako ili uweze kuwa na amani katika maisha yako.
Kutokana na nafasi yetu, hayo kwa leo yanatosha, nitakuwa nikizidi kukupa yale yanayoweza kukufanya uwe bora kwenye uhusiano wako ili uweze kuwa na amani katika maisha yako.
via Global Publishers
No comments:
Post a Comment