VURUGU kubwa za kidini kati ya Waislamu na Wakristo, zimezuka
katika kijiji cha Buseresere, wilaya ya Chato, mkoani Geita, na
kusababisha kifo cha Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of
God, Mathayo Kachila (45), huku watu wengine 10 wakijeruhiwa vibaya kwa
mapanga.
Mchungaji huyo alichinjwa na watu wanaodaiwa ni kuwa waumini wa
Kiislamu kisha mwili wake kutelekezwa kwenye vibanda vya maduka ambavyo
viko jirani na eneo hilo jana.
Taarifa kutoka eneo la tukio hilo zilisema kuwa tukio hilo lilitokea
asubuhi ambapo chanzo chake kinatajwa kuwa ni watu wanaodaiwa kuwa
wafuasi wa Kiislamu kuvamia bucha iliyokuwa ikiwauzia nyama Wakristo wa
kijiji hicho waliokuwa wamepanga foleni kwa wingi kusubiri huduma hiyo.
Wakiristo hao walikuwa wamechinja ng’ombe mmoja na mbuzi wawili eneo
la kanisani kabla ya kuipeleka nyama hiyo katika bucha hiyo iliyoko eneo
la Buseresere Sokoni na ndipo walipokumbana na kadhia.
Mashuhuda walisema kuwa tukio hilo lilianza saa 2:00 asubuhi muda
mfupi baada ya nyama kuwasili katika bucha hiyo ya Wakristo kwa ajili ya
kuuzwa, jambo linalodaiwa kuwakera Waislamu ambao waliivamia bucha hiyo
kwa lengo la kuifunga.
Taarifa ziliongeza kuwa wakati Wakristo wakitafakari uwepo wa Waislamu
kwenye bucha yao, ghafla walishtukia wenzao hao waliokuwa wametapakaa
kwa wingi wakiimwagia nyama hiyo vitu vinavyodaiwa kuwa sumu.
Kutokana na hali hiyo, Wakiristo walioonekana kukerwa na kitendo hicho
na ndipo mapambano yalipoanza kati ya pande hizo mbili huku Wakristo
wakitumia mawe na
Waislamu wakitumia mapanga na majambia.
Ilidaiwa kuwa wakati mapambano hayo yakiendelea, mchungaji huyo ambaye
kwa sasa ni marehemu alifika eneo la tukio ili kujua kulikoni na ndipo
alipojikuta akishambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za kichwani na
kupoteza maisha akikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa
matibabu.
“Yaani ilikuwa kama mzaha tu...baada ya Wakristo kuleta ng’ombe mmoja
na mbuzi wawili kwenye bucha yao, tulishangaa kuona Waislamu wamevamia
hiyo bucha wakati tayari nyama ikiwa inauzwa na Wakristo wakiwa
wamepanga foleni wakisubiri kuhudumiwa,” alisema shuhuda mmoja.
Aliongeza kuwa Waislamu walipofika walitaka kuifunga ile bucha lakini
Wakristo waligoma na ndipo wengine walifika na kuimwagia ile nyama vitu
kama sumu na huo ukawa mwanzo wa machafuko.
“Kwa vile wenzetu walifika eneo hilo wakiwa na silaha tayari walianza
kuwakata Wakristo na kuivunjavunja ile bucha huku Wakristo wakijihami
kwa kutumia mawe lakini walizidiwa nguvu,” alisema shuhuda mwingine.
Waliojeruhiwa ni Saidi Ntahompagaze (45), Sadick Yahaya (40),Yasin
Rajab (56),Vicent Damon (22), wote wakazi wa Buseresere na mtu mmoja
aliyefahamika kwa jina moja la Ramadhan ambaye yuko mahututi katika wodi
namba nane katika hospitali ya wilaya ya Geita.
Hata hivyo watu wengine watano ambao majina yao hayakuweza kupatikana
mara moja walitibiwa na kuruhusiwa kutokana na hali zao kuwa nzuri.
Polisi kutoka wilaya za Chato na Geita walifika eneo la tukio hilo saa
4:30 na kukuta uharibifu mkubwa umekwishafanyika ikiwa ni pamoja na
duka la Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Chato, Yusuph Idd, linalotumika
kwa biashara ya M-Pesa na vinywaji baridi likiwa linateketea kwa moto.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Ludorick Mpogolo, aliyefika eneo la tukio
muda mfupi baada ya polisi kuwasili, mbali na kusikitishwa na kitendo
hicho aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikiangalia njia
sahihi za kutatua mgogoro huo ambao unakua kwa kasi kila kukicha.
Hivi karibuni mgogoro huo wa kidini umezidi kukua wilayani humo kwa
pande hizo mbili kila upande ukidai ndiyo wenye haki ya kuchinja nyama
inayouzwa buchani.
No comments:
Post a Comment