Karibu watu 51 wamekufa kutokana na kunywa pombe ya
kienyeji katika mji mkuu wa Tripoli nchini Libya, maafisa wa wizara ya
nchi hiyo wamesema.
Maafisa hao wamesema watu 378 wamepelekwa katika
hosptali za Tripoli kuanzia siku ya Jumamosi na idadi ya vifo inazidi
kuongezeka.
Maafisa
wa hosptali wameiambia BBC kuwa vifo hivyo vimetokea kutokana na sumu
aina ya methanol na wagonjwa wengi wamefanyiwa tiba ya kuchuja sumu
kwenye figo.
Matumizi na biashara ya pombe ni marufuku nchini Libya lakini inapatikana kwa njia ya siri.
Maafisa wa Wizara ya Afya wamesema watu 38 hadi
sasa wamekufa katika hosptali ya mji mkuu wa Tripoli na wengine 13
walifariki wakati walipokuwa wakisafirishwa kwenda nchini
Tunisia kwa
ajili ya matibabu.
Tayari serikali ya Libya imetangaza hali ya dharura katika mji mkuu wa Tripoli kutokana na tatizo hilo.
Pombe hiyo iliyoleta madhara ni pombe ya kienyeji inayojulikana kwa jina la Bokha. Inatengezwa kwa matunda.
Lakini sumu ya methanol inayotengezwa kiwandani
imekuwa wakati mwingine ikitumika kuongeza ukali wa pombe anaripoti
mwandishi wa BBC Rana Jiwad akiwa Tripoli.
Matatizo yanayotokana na kutumia sumu ya methanol ni pamoja na figo kushindwa kufanya kazi, upofu, kukosa nguvu na kifo.
Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi
hiyo Husein Al Amry ameiambia BBC kuwa kikosi maalum kimezunguka eneo
ambalo pombe hiyo ya kienyeji inapodhaniwa kutengenezwa.
Ameongeza kusema kuwa Wizara inajiaandaa kutumia
nguvu iwapo wamiliki wa eneo hilo hawatakubaliana na amri ya kutoka
ndani ya nyumba.
Pombe ni biashara inayofanywa kwa magendo kutoka Libya kwenda nchi za Tunisia, Algeria na Malta.
No comments:
Post a Comment