MVUA zinazoendelea kunyesha wilayani Bagamoyo, Pwani,
zimesababisha uharibifu mkubwa katika barabara ya Msata–Bagamoyo, katika
eneo la bonde la mpunga na kusababisha magari kushindwa kupita.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika eneo la tukio kushuhudia
hali halisi, mwishoni mwa wiki, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani,
Tumaini Salakikya, aliwataka madereva na wananchi wanaotoka maeneo ya
barabara ya Msata- Chalinze na wanaotoka Bagamoyo mjini kutoitumia
barabara hiyo hadi maji yatakapokauka na barabara kufanyiwa ukarabati.
Alisema kwa sasa wanatakiwa kutumia barabara mbadala ya Mapinga-Vikawe hadi Tamco na Dar es Salaam -Chalinze –Segera.
Aidha alikemea vijana wanaoendelea kufanya biashara za kuvusha watu
kwa malipo ya kati ya sh 1,000 hadi 3,000 kwani ni hatari kutokana na
kutumia kifusi kilichowekwa kutokuwa salama kwao.
Mkuu wa Wilaya ya Bgamoyo, Ahmed Kipozi, aliyefika eneo hilo aliwasihi
wananchi kuacha kung’oa vibao vinavyoonyesha alama ya kufungwa kwa
barabara hiyo na kudai haina msingi kwa maisha ya watu.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Aurich Matei, alisema wanafanya
jitihada za kuelimisha watu kutumia njia mbadala zilizotajwa na kuweka
ulinzi, ili kuepusha madhara.
Barabara ya Msata-Bagamoyo ina urefu wa kilomita 64 ambayo ujenzi
wake umefikia asilimia 90 inatarajiwa kuwa barabara kuu ya kupitisha
magari yatokayo na kwenda mikoa ya ukanda wa kaskazini kutoka Dar es
Salaam. Inajengwa na kampuni ya M/S Estim Contruction Company na
kusimamiwa na M/S H.P Gauff Injeneure GMBH and Company kutoka Ujerumani
kwa gharama ya sh bilioni 89.6.
No comments:
Post a Comment