MTOTO wa kiume, Ikram Seleman, mwenye umri wa miezi minne
ameibwa jijini Dar es Salaam na mwanamke aliyedai kutoka kijiji kimoja
na mama wa mtoto huyo, Zamda Ausi (20).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiyondo, alisema jana kuwa
tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 2:00 usiku, maeneo ya Mbagala
Majimatitu baada ya mama wa mtoto huyo kwenda dukani.
Alisema mtoa taarifa Zamda alieleza kugundua kuibwa kwa mwanaye na
mwanamke anayemtambua kwa sura aliyefika nyumbani hapo siku ya tukio
majira ya saa 10:00 jioni akidai ametokea Mtwara katika kijiji
anachotokea mama wa mtoto.
Kamanda Kiyondo alieleza kwa mujibu wa mtoa taarifa, mwanamke huyo
alipoona mwenyeji wake ametoka kuelekea dukani kununua dawa, ndipo
alipopata mwanya wa kumchukua mtoto huyo aliyekuwa amelala na kutoweka
naye kusikojulikana.
Alisema juhudi za kumtafuta mtuhumiwa na mtoto zinaendelea.
Wakati huohuo, dereva wa pikipiki, Hussrin Saidi (25-30) amefariki
baada ya kugongwa na gari T.771 BRA M/Rosa iliyokuwa ikiendeshwa na
Chedi Alfred.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema ajali
hiyo ilitokea juzi, majira ya saa 7:00 mchana, eneo la Rafia Africana
barabara ya Bagamoyo ambapo dereva wa pikipiki hiyo T 422 BXD aliingia
barabarani bila tahadhari na kugongwa na gari hiyo. Mwili wa marehemu
umehifadhiwa hospitali ya Mwananyamala.
No comments:
Post a Comment