BAADHI ya wananchi wameeleza kusikitishwa na lugha za matusi
zinazoendelea kutolewa bungeni na kuhoji hatua ya kiti cha spika
kutotenda haki katika kutoa adhabu kwa wabunge wa pande zote.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya wabunge kutoleana lugha chafu
wakati wakichangia hoja bungeni hali iliyomfanya Spika wa Bunge, Anne
Makinda, kutangaza kutumia askari kuwatoa nje wale watakaoendelea na
tabia hiyo.
Patrick Enock, mkazi wa Dar es Salaam alisema hatua ya kufanya
upendeleo kwa wabunge inayofanywa na spika na naibu wake haitastawisha
Bunge hilo.
“Spika na naibu wake watende haki ili kuwezesha Bunge kustawi na kwa
kufanya hivyo kutawezesha wabunge kujadili mambo yanayowahusu wananchi
kuliko ya vyama vyao.
“Ukweli kuhusu Bunge, kinachofanyika ni kama Simba na Yanga tu kwani
anayofanya spika ni kama refa ambaye anachezesha mpira na kuegemea
upande mmoja, mfano ni kama jana mbunge aliyetoa tusi zito hajakemewa
wala kutolewa nje. Je, hao wanaotukanwa nao wakae kimya?” alihoji Enock.
Naye Juma Amos, alimwelezea Naibu Spika, Job Ndugai, kuwa ana mfumo kandamizi na kuhoji elimu yake kama inatosha vizuri.
Mwananchi mwingine Ramadhani Rashid alisema inashangaza kuona
utaratibu uliowekwa na spika ukivunjwa wazi wazi tena na naibu wake
aliyekaa kimya wakati Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM)
akitoa tusi zito bungeni.
Alisema ikiwa utaratibu umewekwa hakuna haja ya viongozi kufunika kombe mwanaharamu apite (kunyamazia).
Alieleza kuwa kuna haja kwa vyombo vya habari kuendelea kuibua mambo
yanayotokea ndani ya Bunge ili wananchi waone aina ya wabunge
waliowachagua.
Alikilaumu kituo cha Taifa cha Utangazaji (TBC) kwa kuacha kuonesha
kile kilichoendelea juzi usiku baada ya Naibu Spika kuamuru askari
kuwatoa nje wabunge sita wa CHADEMA.
Wabunge hao ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Highness Kiwia
(Ilemela), Mchungaji Perer Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya
Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana).
Naye Andrew Komu, alisema kuwa vurugu hizo zinatokana na uongozi mbaya
unaoelemea upande mmoja wa Spika Makinda na wasaidizi wake.
Mweka hazina wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu nchini (Shivyawata),
Abdulrahman Lugone, alisema kuwa tatizo lililopo ni kwamba Bunge
linaendeshwa kishabiki zaidi kuliko kuangalia mahitaji ya wananchi.
Aliwataka wananchi kuwa makini katika uchaguzi wa mwaka 2015 kuchagua
wabunge wa maana, wenye akili timamu na viongozi imara wa kuwasaidia.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana,
alisema lugha chafu zinazotolewa na wabunge zinatia kichefuchefu na
hazifurahishi hata kidogo.
Dk. Bana alisema Bunge ni mahali patakatifu hivyo kuna haja kwa wabunge kupaheshimu.
“Nami ni kama wewe sifurahii kinachoendelea bungeni, wabunge watambue
kuwa wao ni waheshimiwa hivyo wana haki ya kulinda hadhi ya uheshimiwa
wao wawapo bungeni na popote pale,” alisema.
No comments:
Post a Comment