Mahakama ya Rufaa imemrejeshea ubunge aliyekuwa mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM)baada ya kung'amua mapungufu ya kisheria katika maamuzi ya Mahakama Kuu iliyokuwa imemnyang'anywa kiti hicho.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliiomba Mahakama ya Rufaa kumrudishia ubunge Hillaly akisema hakuna uthibitisho kwamba alihusika kutoa rushwa wala kufanya vurugu katika kampeni za uchaguzi za mpinzani wake.
Akimwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili wa Serikali Mkuu, Michael Luena akishirikiana na Wakili wa Serikali, Karim Rashid waliomba mahakama itengue hukumu iliyotolewa na Jaji Bethuel Mmila wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga ambayo ilimuondoa madarakani Aeshi.
Aprili 30 mwaka jana, Jaji Mmila alitengua matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Aeshi kutokana na kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, Norbet Yamsebo.
“Waheshimiwa majaji tuna hoja 10 za kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Sumbawanga... katika hoja hizo tutaangalia mambo matatu ambayo yanahusu dhamana ya kufungulia kesi ya uchaguzi, kuwapo vurugu wakati wa kampeni na kuwapo rushwa,” alidai Luena.
Akiwasilisha hoja ya kuwekwa kwa dhamana ya kufungulia kesi kama sheria inavyoelekeza, Wakili Karim alidai kuwa Yamsebo hakuweka dhamana hiyo hivyo anaiomba Mahakama ya Rufani itengue aumuzi uliotolewa wa Mahakama Kuu katika kesi ya uchaguzi.
Kuhusu hoja ya vurugu, Luena alidai kulikuwa na mkanganyiko mkubwa katika ushahidi wa mashahidi wa mlalamikaji (Yamsebo), ambako wengine walidai mkutano wa kampeni ulifanyika lakini wengine walidai haukufanyika kwa sababu ya vurugu.
No comments:
Post a Comment