Habari na Tanzania Daima.
MABOMU ya machozi yaliyopigwa kanisani na tishio la shambulio la
kigaidi jana vilisababisha taharuki kwa waumini na kuvunjika kwa sala
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa
Kunduchi Beach, jijini Dar es Salaam.
Waumini wa kanisa hilo walipatwa kiwewe baada ya bomu la machozi
lililorushwa na polisi kuingia kanisani humo na baadhi ya watu kuanza
kupiga kelele kufananisha hali hiyo na tukio lililotokea wiki iliyopita
mkoani Arusha.
Tukio hilo lilitokea jana saa nane mchana baada ya watu wawili
waliokuwa jirani na kanisa kushukiwa kutaka kufanya uhalifu hivyo baadhi
ya waumini kuamua kuliarifu Jeshi la Polisi.
Awali kabla ya polisi kufika eneo hilo, ilidaiwa watu hao walilenga
kulilipua kanisa hilo kama ilivyofanyika katika tukio lililotokea kwenye
Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti mkoani Arusha
wiki iliyopita ambapo watu watatu walifariki dunia na wengine 70
kujeruhiwa.
Baada ya polisi kupokea taarifa za kuwepo kwa watu wanaotaka kufanya
uhalifu karibu na kanisa hilo la KKKT, walianza kuwashambulia wahusika
kwa mabomu na risasi.
Katika mashambulizi hayo baadhi ya mabomu ya machozi yaliingia
kanisani humo hali iliyowafanya waumini wataharuki huku wengine wakipiga
kelele za kuomba msaada.
Purukushani hizo zilivuruga utaratibu wa sala katika kanisa hilo huku
baadhi ya watu wakieneza taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii
kuwa kanisa hilo limelipuliwa kwa mabomu.
Taarifa hizo zilifanya baadhi ya watu katika Jiji la Dar es Salaam
kuwa na wasiwasi mkubwa huku wakivilaumu vyombo vya dola kwa kushindwa
kutoa ulinzi katika makanisa ambayo yanaonekana kulengwa na mashambulio
ya kigaidi.
Mmoja wa waumini aliyekuwemo kanisani humo, alisema milio ya risasi na
moshi wa mabomu uliokuwamo kanisani humo viliwafanya kukimbia bila
uelekeo maalumu hali iliyozidisha taharuki.
“Baada ya kuhisiwa vibaya watu hao, ghafla polisi walifika eneo la
tukio na kuanza kujihami ikiwemo kurusha mabomu ya machozi ambapo watu
wote tuliokuwa eneo la tukio tuliamua kukimbia.
“Kiukweli tukio lile lilitufanya waumini tuchanganyikiwe sana,
tungeweza kupata madhara makubwa zaidi kwa kukanyagana au kuumia kwenye
viti vilivyomo kanisani,” alisema.
Malasusa agoma kuzungumza
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Kiongozi Mkuu wa KKKT
nchini, Askofu Alex Malasusa juu ya kilichotokea katika moja ya makanisa
yake, lakini aligoma kuzungumzia.
“Nipo kwenye mkutano, siwezi kuzungumzia jambo lolote kuhusu hilo
tishio la ugaidi kama baadhi ya watu wanavyoliita,” alisema.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alikanusha kulipuliwa kwa bomu
kanisani kama baadhi ya waumini walivyodai.
Alibainisha kuwa askari polisi walifika jirani na kanisa hilo na
kuanza kupambana na watu wanaosadikiwa majambazi hali iliyosababisha
hofu kubwa kwa waumini waliokuwemo kanisani.
Kova alisema kuwa askari wake walikuwa kwenye doria ya kawaida ya
kusaka wahalifu na ndipo lilipotokea tukio hilo la kupigwa mabomu hayo
ya machozi.
Kamanda huyo aliwatoa hofu wananchi kuwa hali ya amani katika eneo
hilo na Jiji la Dar es Salaam ni shwari, huku akiwasihi wazipuuze
taarifa za kulipuliwa kwa Kanisa la KKKT.
“Jeshi la Polisi limejipanga kila mahali kuhakikisha vitendo kama
hivyo havitokei, tumewakamata wale tuliokuwa tukiwatilia shaka,” alisema
Kova.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na tishio la kuvamiwa kwa
makanisa mbalimbali mambo yanayochukuliwa kuwa na mlengo wa kidini.
Wiki hii Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti
mkoani Arusha lilipuliwa kwa bomu ambapo watu watatu walifariki dunia na
wengine 70 kujeruhiwa.
Katika tukio hilo la Arusha watu 12 hadi sasa wameshakamatwa wanne kati yao wakiwa ni raia kutoka nchini Saudi Arabia.
No comments:
Post a Comment