JOTO la mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, limezidi
kupanda kiasi cha kila upande kuweka makomandoo wake kuhakikisha hakuna
anayeingia kwenye uwanja huo kwa sababu za kishirikina.
Habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Simba (jina
tunalihifadhi), wao wameamua kuweka mabaunsa 30 kuhakikisha hakuna
‘mtaalamu’ anaingia au kukaribia geti la uwanja huo.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa kazi ya mabaunsa hao ni kufanya uangalizi
kila kona ya uwanja huo kwa nje kuhakikisha hakuna anayeweza kukaribia
mageti.
Mbali ya Simba pia habari hizo zinasema kwa vile kila upande hauna imani na mwingine, Yanga nao wameweka ulinzi.
Habari zinasema kwa upande wa Simba, wameanza kuweka uangalizi rasmi
jana jioni wakihofia wenzao wa Yanga kufika na kufanya mambo yao ya
kishirikina.
“Tumewachukua mabaunsa wa kulinda eneo hilo la uwanja ili mtu yeyote
asiweze kuingia kufanya mambo yake kuelekea mechi ya Jumamosi, si unajua
mechi hizo zilivyo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Ni lazima tufanye hivyo kwa sababu hata wenzetu nao wameweka mabaunsa
wa kutosha, unajua kuna watu hawali wala kulala kwa ajili ya mechi
hii,” kiliongeza chanzo hicho cha uhakika.
Kiliongeza kuwa pamoja na mazingira magumu ya mtu kuweza kuingia
katika Uwanja wa Taifa tofauti na Uhuru, hofu ni kwamba ushirikina
unaweza kufanyika hata kwenye mageti ya kuingilia.
Katika hatua nyingine, chanzo hicho kiliongeza kuwa Kamati ya Utendaji
ya Simba, juzi ilikutana kujadili uteuzi wa mwamuzi wa kati, Martin
Saanya, badala ya Israel Nkongo aliyekuwa amepangwa awali.
Huku wakihoji sababu za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufanya
mabadiliko hayo na wengine wakipendekeza kuliandikia barua Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) ili wapatiwe sababu za mabadiliko hayo.
Nkongo ni mwamuzi aliyewahi kupata kichapo kutoka kwa wachezaji wa Yanga ilipocheza na Azam katika msimu uliopita.
Wakati sarakasi hizo zikiendelea, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts,
alisema kikosi chake kiko tayari kwa mechi hiyo na kuongeza hana shaka
dhidi ya Simba.
“Nawajua vema vijana wangu, mechi ni dakika 90, ngoja tusubiri kuona itakuweje baada ya dakika 90,” alisema Brands.
Aidha tiketi za mechi hiyo zitaanza kuuzwa leo katika vituo mbalimbali
jijini Dar es Salaam ambavyo ni Uwanja wa Taifa, Mgahawa wa Steers,
Mtaa wa Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Oilcom
Ubungo, kituo cha mafuta Buguruni, BMM Barbershop Sinza Madukani, Dar
Live Mbagala na Sokoni Kariakoo.
Timu hizo zitakutana katika mechi hiyo ya kufunga msimu wa 2012/13
huku Yanga ikiwa bingwa ikifuatiwa na Azam katika nafasi ya pili na
Simba ya tatu.
Kwa upande wa Yanga, ni ubingwa wa 24 tangu kuanza kwa ligi hiyo mwaka 1965, wakati huo ikiitwa Ligi ya Taifa.
Viingilio vya mechi hiyo ni sh 5,000 kwa viti vya kijani; sh 7,000
viti vya bluu; sh 10,000 viti vya rangi ya chungwa; sh 15,000 VIP C; sh
20,000 VIP B; na sh 30,000 kwa VIP A.
No comments:
Post a Comment