MBUNGE wa Mbozi Magharibi, David Silinde (CHADEMA), ameitaka
serikali ieleze ni lini itamaliza zoezi la uandikishaji wa vitambulisho
vya taifa.
Silinde alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la
nyongeza ambapo alisema zoezi la uandikishaji wa vitambulisho hivyo
limekuwa likiendelea na mpaka sasa hivi ni viongozi pekee ndio
waliopata.
“Sasa napenda kujua kauli ya serikali kwa sababu vitambulisho hivi
vinaweza kutumika kwenye kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Je, ni lini serikali itamaliza zoezi hili la uandikishaji wa
vitambulisho vipya ili wananchi wote waweze kupata vitambulisho hivi?”
alihoji Silinde.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, akijibu
swali hilo alikiri kuwa kasi inayotumika kwa ajili ya uandikishaji wa
vitambulisho ni tofauti na walivyoitegemea huku akibainisha kwamba jumla
ya watu milioni 2.7 wameandikishwa.
Hata hivyo, serikali ilipanga zoezi hili limalizike mwakani na
vitambulisho hivyo viwe ni sehemu ya mchakato wa kupiga kura na matumizi
mengine.
“Kweli kuna tatizo…na tatizo hasa lipo kwenye bajeti, mahitaji ya NIDA
kwa ajili ya shughuli hii hayafikiwi kwenye bajeti,” alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa
(CUF) alitaka kujua kama raia wa nchi nyingine hawawezi kuvipata
vitambulisho vya taifa na iwapo zoezi la kuhesabu watu halikuwagusa raia
wa kigeni.
Naibu waziri alisema: “Ni kweli kuwa nchi yetu imezungukwa na nchi
zenye migogoro, hivyo kutoa viashiria vya kuweza kuandikisha watu
wasiostahili.”
Alisema katika kuhakikisha kuwa hawaandikishi watu wasiohusika,
serikali imepeleka madaftari ya wakazi yanayoratibiwa na serikali za
mitaa ambayo lengo lake ni kuandikisha wakazi wote wa kila kaya na
kuhifadhi taarifa zake.
No comments:
Post a Comment