WAREMBO wanaowania taji la Redd’s Miss Kinondoni 2013/2014,
jana wamefanya usafi hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam
pamoja na kujionea hali ilivyo mbaya kwa wagonjwa.
Akizungumza baada ya kumaliza usafi huo, Redd’s Miss Kinondoni
anayemaliza muda wake, ambaye pia ni Miss Tanzania, Brigite Alfred,
alisema wameamua kufanya hivyo wakiwa na lengo la kufanya harambee ya
kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua vitanda kwa ajili ya wodi ya
akina mama wanaojifungua.
Alisema harambee hiyo itafanyika keshokutwa kwenye Ukumbi wa
Ambassador Lounge Posta jijini Dar es Salaam ambako Meya wa Manispaa ya
Kinondoni, Yusuf Mwenda, anatarajia kuwa mgeni rasmi.
“Huu ni mwanzo tu, bado tunaendelea kutembelea hospitali mbalimbali,
leo tumeanza Mwananyamala kesho tutakuwa hospitali ya Sinza pamoja na
kutembelea mradi wa mabasi yaendayo kasi,” alisema mrembo huyo.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Gunin Kamba, aliwashukuru
waandaaji wa mashindano hayo kwa harambee hiyo, ambayo itasaidia afya
za wagonjwa wa hospitali hizo kwa kiasi fulani.
“Mimi naomba wananchi wengine waige mfano huu, kwani jukumu la usafi
ni la kila mtu, sio kuisubiri serikali peke yake, naomba liwe zoezi
endelevu lisiishie hapa,” alisema Dk. Kamba.
Mashindano ya Redd’s Miss Kinondoni yanatarajiwa kufanyika Juni 21 na
yamedhaminiwa na Redd’s Original, Chilly Willy energy drink, Oriflame
Natural Beauty Products, Times Fm na Jb Belmont Hotel.
No comments:
Post a Comment