LOS ANGELES, MAREKANI
HAKUNA shabiki wa muziki ambaye anaweza kutoka mbele na kusema halifahamu jina la Rihanna.
Nyota huyo mwenye sauti tamu na sura ya kupendeza, anawika duniani kote na amekuwa akivuna mashabiki kila kukicha.
Mashabiki wanavyoongezeka ndivyo dada huyo aliyezaliwa miaka 25 iliyopita huko Saint Michael, Barbados anavyoongeza utajiri, hiyo ni kwa kuwa nakala za albamu zake hununuliwa zaidi.
Kwa mujibu wa mtandano wa The Richest, Rihanna ambaye pia ni mwigizaji, ana utajiri wa dola 60 milioni mpaka kufikia Desemba 2012.
Awali mwanamuziki huyo alikuwa hafahamiki, lakini maisha yake yalibadilika baada ya rafiki yake mmoja kumkutanisha na Evan Rodgers, prodyuza kutoka New York.
Prodyuza huyo alikuwa katika mapumziko ya kawaida huko Barbados akiwa na mke wake ambaye ni mwenyeji wa eneo hilo.
Baada ya kutambulishwa, Rodgers alimsikiliza na alikubali kuwa mwanamuziki huyo ni mkali na alimtaka afike New York ili akutane na Jay-Z, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya kurekodia ya Def Jam.
Jay-Z alimsikiliza anavyoimba na kufahamu kuwa Rihanna hakuwa na sauti ya kawaida, alikuwa na nyota ya pekee. Wakati huo alikuwa na miaka 16 tu lakini alisaini mkataba na Kampuni ya Def Jam.
Alianza kwa kutoa albamu kali ya ‘Music Of The
Sun’ mwaka 2005, ambapo dada huyo aliuza mamilioni ya nakala. Albamu
yake ya pili ‘A Girl Like Me’ ambayo ilikuwa na singo kali ya ‘S.O.S.’
ilikamata soko mwaka 2006 na kuuzwa nakala nyingi.
Mwaka huo pia alitoa albamu ya ‘Don’t Stop Til You Get’. Mwaka 2008 alitoa albamu ya ‘Good Girl Gone Bad’ na mwaka uliofuata alitamba na albamu ya ‘Rated R’. Mwaka 2011 akatikisa na albamu ya ‘Talk That Talk’ na mwaka jana akalipuka na albamu ya Diamonds.
Licha ya kuvuna utajiri mkubwa kwenye nyimbo, Rihanna pia alianza kuigiza tangu mwaka 2006 wakati alipotoa filamu ya ‘Bring It On: All or Nothing.’ Huku akiwa ameuza albamu zaidi ya nakala 25 miloni na kuuza singo zaidi ya 60 milioni duniani kote, mwaka jana Billboard ilimtangaza kuwa mwanamuziki bora wa digitali wa muongo mmoja.
Dada huyo pia ana ubia na makampuni ya Clinique, Reebok, Vita
Coco, Nivea na Secret. Vile vile anamiliki kampuni ya manukato ya Reb’l
Fleur, vyote hivyo vinamwingizia kiasi kikubwa cha fedha.
Dada huyo pia huwa hachoki kuzunguka kupiga shoo kali na mwaka 2011-2012 pekee alipiga shoo 85 kwenye nchi mbalimbali duniani.
Mwaka 2012, Jarida la Forbbes lilimtangaza kuwa
ameshika namba nne kwa utajiri miongoni mwa wanamuziki. Dada huyo ana
mashabiki 53 milioni kwenye facebook, anashika namba mbili nyuma ya
Eminem kwa upande wa wanamuziki.
Maisha binafsi
Licha ya utajiri mkubwa, Rihanna, amekuwa mtumwa
wa mapenzi kwa mwanamuziki wa R&B, Chris Brown. Rihanna alikuwa na
uhusiano mzuri na Brown kwa miezi kadhaa, lakini mwaka 2009 kijana huyo
alimpiga na kumuumiza vibaya kwa kile kilichodaiwa ‘kisa cha mapenzi’.
Brown alikutwa na hatia na alihukumiwa kufanya kazi za jamii na kuwa
chini ya uangalizi maalumu kwa miaka mitano. Kabla ya miaka ya adhabu
kukamilika, dada huyo alikiri bado anampenda kijana huyo na walirudiana
tena. Hata hivyo hivi karibuni Brown alisema hamtaki binti huyo. Licha
ya muziki, sifa kubwa ya dada huyo ni kubadilisha staili za nywele ikiwa
ni pamoja na rangi.
“Ninapenda kubadilisha nywele, nadhani zinanipa muonekano mpya,” alisema dada huyo ambaye mwili wake una tatoo 18.
Mwanamuziki huyo anaishi kwenye nyumba ya kifahari nyenye thamani ya pauni 12 milioni huko Pacific Palisades, Los Angeles.
No comments:
Post a Comment