Nimepokea ujumbe kwenye anwani pepe yangu lakini nikautilia mashaka na kuutuma kwenye kapu la 'spam' kutokana na yaliyoandikwa humo kuwa ni yale yale yanayoandikwa kwenye ujumbe wa kujaribu kuwarubuni, kuwahadaa na kisha kuwatapeli watu fedha, mali na hata kuwadhuru wanapokutana ana kwa ana.
Ujumbe huu ninauweka hapa ili kuwasaidia wengine ambao wanaweza wakatumiwa pia na kufikiri unatoka kwenye shirika kubwa linalohusika na masuala ya Usalama wa Taifa la Marekani, FBI.
Mambo muhimu ya kutizama kama ambavyo nimeeleza siku na miaka iliyotangulia, ni:-
- Dalili ya mwanzo kabisa ya kutambua utapeli ni maombi ya kutuma taarifa zako binafsi kama vile, vielelezo na majina yako rasmi na kamili unayoyatumia kwenye vitambulisho na pasi ya kusafiria, umri, nchi unamoishi, anwani ya posta, anwani ya mahala unapoishi, kazi uifanyayo, nambari za simu, maelezo ya akaunti za benki (hasa hufanyika unapowajibu na wakakuahidi kuwa wanataka sasa kukutumia fedha hivyo uwape taarifa hizo) na mengineyo. Inawezekana wakadai sehemu tu ya taarifa nilizotaja hapa au hata zaidi, leng ikiwa ni kukuvuruga kiakili na uamini watu hawa wapo makini kwa kudai vielelezo vyote hivyo.
- Kwenye Gmail, bofya kimshale kilichopo punde tu baada ya anwani ya mtumaji kwenda kwa mpokeaji (To:) ili kuona endapo anwani ya mtumaji na anwani ambayo inapaswa kupokea majibu ya 'reply' zinaoana (tizama kielelezo nilichopachika hapo chini). Anwani hizo zikipishana, ni dalili kubwa kuwa ujumbe huo ni wa kuhadaa. Ingawaje anwani hizo zinaweza kutofautiana na ujumbe ukawa wa kweli, mara nyingi hii hutokea endapo mtu mnayewasiliana mara kwa mara anatumia zaidi ya anwani moja lakini amepanga majibu ya ujumbe wake yawe yanapokelewa kwa anwani fulani tu.
- Ukitizama kwenye "To" ukaona pako peupe (blank) ni dalili kuwa ujumbe huo umetumwa kwa watu wengi kwa kutumia "Bcc" field na ni rahisi sana kuwa umetumwa kwa kubahatisha anwani ambazo zipo hai (active accounts). Hii ni njia nzuri ya kukufahamisha kuwa endapo ujumbe huu ungekuwa unakuhusu binafsi, anwani yako ingeonekana kweney "To" field kama ujumbe mwingine. Vile vile kitendo cha kutuma kwa watu wengi ujumbe wa ushindi ama urithi wa kiwango kikubwa cha fedha ni cha kutilia shaka kwa kuwa maelezo yameelekezwa kwa mtu mmoja wakati ujumbe umetumwa kwa watu wengi. Ingekuwa ushindi umepatikana kwa watu wengi, maelezo yote yangebainisha hivyo. Vile vile haiwezekani kushinda fedha nyingi bila ya kutangazwa rasmi kwenye vyombo vya habari.
- Mnaojua au mnaotaka kujifunza kwa kiasi fulani kuchunguza chanzo na njia ilikopita ujumbe uliotumiwa, bofya kimshale kilichopo baada ya neno "reply" (Gmail) kisha chagua neno "Show original" ambayo itafungua kidirisha chenye maelezo ya kina (header) yatumie haya ku-trace ujumbe wako na kuoanisha anwani zilizotumika kwenye "to", "path" na "from" ili kuona kama kuna uwiano ama mpishano mkubwa. Unaweza kuchunguza (analyse header) kwa kutumia tovuti huru (mfano bofya hapa kuona hizi zilizoorodheshwa kwenye google.com)
- Tizama matumizi ya lugha. Ikiwa lugha iliyotumika ni tofauti na lugha unayozungumza, mathalani, unazungumza Kiswahili na Kiingereza lakini ujumbe umekuja katika lugha ya Kifaransa ama Kireno, hiyo ni dalili tosha kuwa aliyekuandikia hakufahamu la sivyo angetumia lugha mojawapo ya zile unazozitumia katika nchi unayoishi.
- Tizama sarufi iliyotumika. Inawezekana pia lugha ikatumiwa ile ambayo umeizoea, lakini ikawa ina makosa kisarufi. Mara nyingi matapeli wa mtandaoni hutumia mashine za kufasiri lugha bila kujua kilichofasiriwa kama kimekuwa tafsiri halisi na yenye maana ama la. Ukiona hilo pia jua ni dalili kubwa ya utapeli.
- Tizama muundo wa ujumbe. Inawezekana katika kuandishi zikatumika alama za mshangao (!!!) zaidi ya moja kwa wakati mmoja ama kutumia HERUFI KUBWA zilizokolezewa wino na kubadilishwa rangi ya maandishi na hata kuchora mstari chini ya maneno, ili kuweka msisitizo. Mara nyingi hii si kanuni (ethics) ya uandishi wa barua rasmi za kiofisi isipokuwa tu kwenye vichwa vya habari ama inapolazimu kufanya hivyo.
- Dalili nyingine kubwa ya kutizama ni endapo kuna 'link' katika ujumbe uliotumiwa, chunguza link hiyo kwa kuweka pointer ya mouse juu ya maandishi ya link hiyo bila kubofya (DO NOT CLICK, just hover your mouse over) na kisha tizama chini kushoto mwa kioo cha (window screen) computer yako kisha ulinganishe endapo kinachosomeka kwenye ujumbe huo kinaoana na kinachosomeka kushoto mwa screen yako. Mathalan, naweza hapa naandika "bofya hii link kuona ndani ya Ikulu ya Rais http://www.ikuluyarais.com lakini ukibofya maandishi ya link hii haitakupeleka kwenye tovuti ya Ikulu ya Rais kuona ndani mwake kama nilivyosema, bali itakupeleka kwenye blogu yangu ya awali, kwa kuwa ndicho nilichokificha chini yake.
- Ikiwa una muda, unaweza kutafuta mawasiliano ya ofisi au mtu anayetumiwa kutapeli na kuwapigia kuwafahamisha kuhusu utapeli huo, ili wajue kinachoendelea na kwamba wanatumika vibaya ili waweze kutoa angalizo la kuwasaidia watu wengine wasihadaiwe. ZINGATIA: Usitumie namba za mawasiliano zilizoandikwa kwenye ujumbe uliotumiwa. Tafadhali sana usifanye hivyo kwa maan mawasiliano ya simu hapo karibu mara zote huwa yanapokelewa kwenye ofisi za matapeli hao hao kwa kuigiza uhalisia)
No comments:
Post a Comment