JESHI
la Polisi mkoani Arusha, jana lilimuweka chini ya ulinzi kwa muda wa
saa tano Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema),
kwa tuhuma za kumshambulia aliyekuwa wakala wa CCM, Hussein Warsama,
wakati wa uchaguzi mdogo Kata ya Makuyuni, Monduli.
Mbunge huyo hivi karibuni alidai kujeruhiwa wakati akishiriki katika uchaguzi huo, alikwenda kituo cha Polisi mjini Arusha baada ya kupigiwa simu na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Makao Makuu, Kamishna Isaya Mngulu, aliyeomba waonane na baada ya kufika alijikuta akiwekwa chini ya ulinzi.
Akizungumzia tukio hilo, Nassari alisema Kamishna Mngulu alimpigia simu juzi akiomba waonane, hata hivyo hawakuweza kukutana naye na hivyo kumuomba waonane jana.
Alisema baada ya kushindikana kuonana juzi, huku akiwa hajui alichoitiwa, jana alipokea simu ya Kamishina Mngulu akiomba wakutane, hatua iliyomfanya ashangae kwa kuwa ilikuwa ni siku ya mapumziko.
“Aliponipigia nilishangaa, nikamuuliza mbona leo ni siku ya mapumziko unafanya kazi? Nilidhani ilikuwa ni (issue) jambo la kijamii, hivyo nikaamua kumsikiliza.
“Nikiwa kituoni nilipokelewa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO) Nyanda na kisha akaniweka chini ya ulinzi,” alisema Nassari kwa mshangao.
Alisema baada ya kuwekwa chini ya ulinzi
aliomba kujulishwa makosa yanayomkabili, ambapo alielezwa kuwa
anakabiliwa na tuhuma za kushambulia watu wilayani Monduli.
Alisema
baada ya kujulishwa tuhuma hizo, ndipo walipomtaka aandike maelezo
yake, hatua ambayo aliikataa akidai hakuwa tayari kufanya hivyo kwa
sababu hakujua alichoitiwa.
“Nimegoma kuandika maelezo yangu, nimewaambia sina maelezo ya kuandika. Sikujua nakuja kufanya nini polisi.
“Nimewaambia
mpaka nitakapokuwa na mwanasheria wangu, nilimtafuta Mabere Marando
sikumpata, nikamtafuta Tundu Lissu sikumpata pia.
“Baada ya kuwakosa wote ndipo wakaanza kuniambia niwekwe ndani, nikawaambia sawa, hivyo nikavua saa na miwani yangu.
“Nilipovua
vifaa vyangu, wakabadilisha mawazo wakasema nipelekwe Monduli. Askari
mwingine akasema gari haina mafuta, nikiwa nasubiria wafanye nini
Kamishna Mngulu aliwasili na kutoa maagizo ya kunitaka nijidhamini
mwenyewe.
“Tangu saa 2 asubuhi walikuwa wananishikilia hadi Saa 6
mchana walipoamua kuniachia kwa kujidhamini mwenyewe, wakisema eti
watanipigia simu,” alisema Nassari.
Nassari alionyesha kushangaa
hatua ya polisi kumuweka chini ya ulinzi kwa tuhuma za kumshambulia
Warsama, huku akidai kuwa yeye ndiye aliyenusurika kutekwa na kupigwa na
watu aliodai kuwa ni wafuasi wa CCM siku ya uchaguzi huo, ambao Nassari
alikwenda kwa ajili ya kusimamia na kuwa wakala wa mgombea wa Chadema,
Japhet Sironga.
Hata hivyo kwa upande wake RCO Nyanda,
alipotafutwa kuzungumzia suala hilo aligoma, akidai kuwa atafutwe
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ambaye ndiye msemaji wa jambo hilo.
“Naelekea Dodoma, mtafute RPC ndiye msemaji wa Polisi Mkoa,” alisema RCO Nyanda kwa njia ya simu.
Taarifa
za kiintelijensia zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa Nassari
alianza kutafutwa na askari wa polisi tangu Julai 23, mwaka huu, huko
wilayani Arumeru, ambapo jeshi hilo lilikuwa likisubiri amalize matibabu
kisha limhoji.
Wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya
Makuyuni, wilayani Monduli, Nassari anadaiwa kumpiga wakala wa CCM
aliyejulikana kwa jina la Warsama au Msomali.
Ilidaiwa kuwa hatua
hiyo iliibua hisia kwa vijana wa Kimasai (Morani), walioanza kumsaka
mbunge huyo ambapo alijikuta akijeruhiwa shingo na hivyo kusababisha
kulazwa Hospitali ya Selian Arusha, kisha Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Dar es Salaam.
VIA MTANZANIA
No comments:
Post a Comment