Daktari wa rais Kikwete, Profesa Mohammed Y. Janabi.
Profesa
Mohammed Y. Janabi, Daktari wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanikiwa kuingia katika kundi dogo
la madaktari wa Afrika waliothibitisha kuwa na ujuzi na utaalam wa
kuwapima na kutoa liseni za vipimo vya afya kwa watumishi wa anga
wakiwamo marubani.
Katika barua ambayo aliipokea Dkt. Janabi wakati anaandamana na Rais
Kikwete katika ziara ya kikazi ya Marekani na Canada iliyomalizika
Jumamosi, Septemba 28, 2013, Wizara ya Usafirishaji ya Marekani kupitia
Utawala wa Shughuli za Anga wa Marekani (FAA) imesema kuwa imemteua
Profesa na Dkt. Janabi kuwa Daktari wa Shughuli za Anga (AME) kuanzia
Agosti 14, mwaka huu, 2013.
“Uamuzi huu una maana kuwa sasa unaweza kuwapima na kuendesha
shughuli za kitibabu na kutoa ama kukataa kutoa liseni ya kuthibtisha
afya za watumishi wa sekta ya anga wakiwemo marubani wa ndege za
usafirishaji, wa ndege za biashara za abiria, marubani wa ndege binafsi
na marubani wanafunzi.
Profesa Janabi anakuwa daktari wa 31 katika Afrika na wa tatu katika
Afrika Mashariki kupatiwa hadhi hiyo ambayo inapatikana baada ya kazi
ngumu ambayo ni pamoja na kufanya mtihani maalum.
Nchi pekee katika Afrika Mashariki iliyokuwa na madaktari wa kiwango
hicho kabla ya Dkt. Janabi kuingia katika kundi hilo ni Kenya yenye
madaktari wawili. Tanzania sasa inakuwa nchi ya pili katika Afrika
Mashariki kuwa na hadhi hiyo.
Kwa upande wa Afrika, Profesa Janabi anaungana na madaktari kutoka
Burkina Faso (1), Cameroun (2), Misri (6) ambayo ndiyo madaktari wengi
zaidi katika kundi hili, Ghana (1), Libya (1), Morocco (1), Nigeria (5),
Ethiopia (4), Kenya (2), Afrika Kusini (5) kukubaliwa kuifanya kazi hii
ya kimataifa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Septemba, 2013
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Septemba, 2013
No comments:
Post a Comment