Habari na Zawadi Chogogwe wa Tanzania Daima.
MADIWANI wa Halmashauri ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wamelaani
kitendo cha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufika katika vijiji
vya Bagamoyo na kuwatumikisha wananchi kazi za miradi mbalimbali huku
fedha wakichukua wao.
Madiwani hao waliibua hayo mjini Bagamoyo juzi katika kikao cha baraza
la madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2012 na 2013 kilichofanyika
katika ofisi za mkurugenzi wa halmashauri hiyo ambacho kilihudhuriwa na
wataalamu mbalimbali.
Diwani wa Kilomo, Hassan Usinga, alisema Tasaf wamekuwa na tabia ya
kutofika kwa watendaji wa vijiji pindi wanapofanya kazi zao za miradi
na badala yake wanaenda moja kwa moja kwa wanakijiji na kuwatumikisha
katika miradi ya maendeleo huku wakiwalipa fedha kidogo.
“Kitendo cha kwenda kwa wanakijiji kuwafanyisha kazi na kuwalipa fedha
kidogo kumechangia miradi mingi kuwa mibovu huku mingine ikiwa imekufa
kama vile miradi ya kuku,” alisema Usinga.
Alisema taarifa za maendeleo ya vijiji zinaonyesha kuwa dawa za mifugo
na matumizi zimetolewa kwa wanakijiji na kueleza kuwa taarifa hizo
zikiwa hazina ukweli.
“Kutowashirikisha watendaji wa vijiji katika mikutano ya maendeleo
kumepelekea kukosa wanakijiji wengi kushiriki katika mikutano yao,”
alisema.
Alisema wanaoshiriki wanakuwa wachache hali inayowafanya Tasaf
kuwavalisha fulana na kofia huku wakiwapiga picha na kuzipeleka kwa
wafadhili kwa kuonyesha ushahidi kuwa wanakijiji wameshiriki mkutano huo
wakati sio kweli.
Aliongeza kusema sh milioni 27 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo ya
barabara za
Tukamisasa kwenda Mbuyu, katika kata ya Ubena lakini cha
kushangaza barabara hiyo haijajengwa kwa kiwango kutokana na wananchi
kulazimika kuitengeneza kwa majembe baada ya kuona hakuna juhudi zozote
za mamlaka husika.
“Tunaiomba Tasaf iache kutuchezea mchezo mchafu sisi watu wa
Bagamoyo kwa kuwatumia wanavijiji kwa manufaa yao wenyewe,” alisema.
Wakati huohuo, madiwani hao walilalamika kuwa watumishi wa halmashauri
hiyo hawana nyumba za kuishi za kiofisi, hali inayowafanya waishi
katika nyumba za kupanga.
Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Fukayosi, Ally Issa, alisema
inatia aibu kuona watumishi wa Halmashauri ya Bagamoyo wakiishi katika
nyumba za kupanga badala ya nyumba za kiofisi.
“Halmashauri inakusanya mamilioni ya fedha lakini inashindwa
kuwajengea watumishi wake nyumba za kuishi. Mkurugenzi acha mambo ya
siasa tunachotaka ni kuona nyumba za watumishi zinajengwa na
kukabidhiwa,” alisema Issa.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Samwel Sariaga, alisema katika bajeti
ya mwaka huu watajenga nyumba nne za watumishi ambazo kila moja
itagharimu sh milioni 40.
Katika hatua nyingine, madiwani hao wametishia kuiburuza Bima ya Afya
mahakamani, kwa kitendo cha kuwakata asilimia 5 kila mwezi ndani ya
miaka mitatu bila kuwapatia kadi za matibabu.
Diwani wa Viti Maalum, Hapsa Jumam, alisema wakati wanaingia
madarakani waliahidiwa watapewa kadi za matibabu, lakini cha kushangaza
mpaka sasa hawajapewa.
No comments:
Post a Comment