WALIOKUWA wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Weruweru
iliyopo Kilimanjaro kwa kushirikiana na bodi ya shule hiyo wameandaa
sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ambayo yatafanyika Septemba 21, mwaka
huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati ya
maadhimisho hayo, Mwanaidi Maajar, alisema kuwa maadhimisho hayo
yatafanyika sambaba na uchangishaji wa fedha za ukarabati wa majengo
yaliyoharibika pamoja na ujezi wa bweni jipya.
“Katika ziara ya kutembelea Shule ya Weruweru hivi karibuni
ilidhihirika kwamba majengo ya shule hiyo yenye miaka 50, yamechakaa,
hivyo basi ili kurejesha heshima ya mama mlezi kama sehemu ya
maadhimisho Wana Weruweru wataanzisha chama chao kwa kuzindua mfuko
maalumu wenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajiri ya kurejesha hadhi
ya shule yetu hiyo ili iendane na karne ya 21, ” alisema.
Mwanaidi aliongezea kuwa, zinahitajika sh milioni 500 kwa kuanzia, ili
kufanikisha ukarabati wa majengo ya shule hiyo, pamoja na ujenzi wa
jengo jipya la bweni..
Hata hivyo, tayari Wana Weruweru wameishaanza kuchangia, hivyo
aliwaomba marafiki na wapenda maendeleo ya elimu kujitolea kudhamini kwa
kutangaza katika Jarida Maalumu la miaka 50 ya Weruweru kwa michango,
ama kwa kununua kanga au kwa kutuma fedha kwa kutumia namba 0713 213
771 Tigo, 0763 475 506 Voda na 0786 213 771 Airtel.
Maadhimisho hayo yatakutanisha wageni takriban 2,500 wakiwamo viongozi
mbalimbali wa serikali, wanafunzi na wazazi na mgeni rasmi katika
sherehe hizo ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
No comments:
Post a Comment