Juma Kaseja.
KOCHA wa makipa wa kikosi cha
Taifa Stars, Juma Pondamali, ameshangazwa na uwezo wa kipa wake namba
moja, Juma Kaseja, licha ya kutokuwa na klabu yoyote kwa sasa.Kaseja ambaye tangu alipotemwa na Simba hajafanikiwa kupata timu, alimjumuishwa katika orodha ya kikosi cha Stars kilichopo kambini kikijiandaa na mchezo dhidi ya Gambia utakaopigwa Jumamosi ijayo jijini Banjul, Gambia.
Akizungumza Pondamali amesema tangu kikosi hicho kianze mazoezi mwishoni mwa wiki iliyopita, Kaseja ameonyesha uwezo mkubwa wa kudaka huku akiwazidi baadhi ya makipa wenzake ambao wametoka katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
Pondamali ambaye ni kipa wa zamani wa kikosi hicho cha Stars, amesema mbali na uwezo huo wa Kaseja, pia kipa huyo na nahodha wa kikosi hicho, ameonyesha kuwa mwepesi, jambo ambalo linaashiria alikuwa akijifua vizuri.
“Hajaonyesha tofauti yoyote mpaka sasa tangu ajiunge na timu, niliwapa mazoezi kadhaa tofautitofauti lakini Kaseja alifungwa mabao mawili huku wengine wakifungwa sita, kitu ambacho kilinishangaza, nikawauliza wenzake kwa nini wanafanya vibaya kuliko Kaseja, wakanijibu wana uchovu wa safari,” alisema Pondamali.
“Ukiacha hilo, pia bado ameonekana mwepesi zaidi, ukiwa nje ya timu mara nyingi tunahofia unaweza kuongezeka uzito kutokana na kutokuwa na ratiba ya kutosha ya mazoezi, lakini Kaseja ameonekana kuwa sawa, inaonyesha alikuwa akijifua kwa mazoezi binafsi,” aliongeza.
Kaseja alikuwa amekaribia kujiunga na FC Lupopo ya DR Congo lakini dili hilo likafa kutokana na baadhi ya watu kudaiwa ‘kumchomea utambi’.
CHANZO NI GLP
No comments:
Post a Comment