ZAIDI ya wasichana 55,000 wa shule za msingi na sekondari Tanzania Bara, wamekatisha masomo yao kwa sababu za ujauzito.
Licha ya kukatisha masomo, wasichana hao walitengwa na jamii baada ya
kupata ujauzito na kuwaharibia mtiririko bora wa maisha yao katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Hayo yalibainika Dar es Salaam juzi usiku wakati wa uzinduzi wa
ripoti ya utafiti namna Wasichana wa shule nchini Tanzania
wanavyofanyiwa kwa nguvu vipimo vya ujauzito na kufukuzwa wanapokutwa
wajawazito.
Utafiti huo ulifanywa na Kituo cha Kutetea Haki ya Uzazi kiitwacho
Centre for Reproductive Rights kati ya mwaka 2012/2013 na kubainisha
hayo huku ukieleza kwamba asilimia 44 ya wasichana Tanzania Bara
wamepata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 19 huku wengi kati yao
wakitengwa na jamii.
Akizungumzia utafiti huo mkurugenzi mkazi wa kituo hicho kanda ya
Afrika Evelyne Opondo alisema utafiti huo umehusisha shule za bweni za
serikali na binafsi.
“Tumegundua kwamba wakuu wa shule wanawapima mimba wananfunzi kwanza
kwa njia za kienyeji, pili wanafanya hivyo bila kujua kwamba hakuna
sheria wala sera inayowaruhusu kuwapima mimba wanafunzi hao.
“…Lakini wakuu wa shule na serikali za maeneo hayo wanafanya hivyo
bila kujua hawaruhusiwi,” alisema Evelyne huku akisisitiza kwamba
hakuna sheria inamwadhibu mtoto wa shule kwa kumzuia kuendelea na
masomo huku ikiwa bubu kwa aliyemtia ujauzito huo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Baraza la Afrika la Haki na Usawa
wa Mtoto Dk. Clement Mashamba alisema hakuna utaratibu sahihi wa
kisheria wa kumwajibisha aliyemtia ujauzito mwanafunzi huku akishauri
kuwepo na mfumo mmoja wa kuwaadhibu wanaume hao.
No comments:
Post a Comment