MALIKIA wa taji la Redd’s Miss Tanzania 2013 anatarajiwa
kuondoka na gari dogo lenye thamani ya sh milioni 15 sambamba na kitita
cha sh milioni nane.
Shindano hilo linalotarajiwa kushirikisha warembo 30 kutoka sehemu
mbalimbali hapa nchini, limepangwa kufanyika Septemba 21, mwaka huu,
kwenye ukumbi wa Mlimani City, huku likipambwa na burudani za kila aina
kutoka kwa wasanii maarufu wa ndani na nje.
Akitangaza zawadi hizo jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji
cha Redd’s Original, Victoria Kimaro, alisema wameamua kutangaza mapema
zawadi hizo ili kuleta morali kwa washiriki wa shindano hilo.
“Tunaamini shindano la mwaka huu litakuwa na ushindani mkubwa zaidi na
zawadi hizi zitakidhi kwa kiasi kikubwa mahitaji ya warembo,” alisema
Victoria.
Mbali na mshindi kutwaa zawadi hizo, mshindi wa pili atapata sh
milioni 6.2, wa tatu sh milioni nne, wa nne sh milioni tatu, wa tano sh
milioni mbili, huku mshindi wa sita hadi 15 watapata sh milioni 1.2
kila mmoja na waliobaki watajipoza kwa sh 700,000 kila mmoja.
“Thamani ya fedha taslimu itakuwa ni sh milioni 46.1 na zawadi zote
hizi watakabidhiwa warembo wa Redd’s Miss Tanzania siku inayofuata baada
ya kufanyika kwa fainali hizo,” alisema Victoria.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim
Lundenga, ambao ndio waandaaji, aliwashukuru wadhamini na kusema,
wamefanya kazi kubwa zaidi katika kuyakuza mashindano hayo.
“Kwa mara nyingine tunapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wadhamini
wetu wakuu Redd’s Original na wadhamini wenza, ambao kwa kweli
wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa
zuri zaidi,” alisema Lundenga.
Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte
Alfred, aliyelitwaa taji hilo mwaka jana na kukabidhiwa gari aina ya
Noah, pamoja na kitita cha sh milioni nane.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original.
No comments:
Post a Comment