NILIWAHI kuzungumzia kuhusiana na Coastal Union kuachana na malumbano yasiyokuwa na sababu dhidi ya aliyekuwa mdhamini wao, Nassor Bin Slum ambaye ni mnazi mkubwa wa timu hiyo.
Azim Dewji.
Mwisho Bin Slum ameondoka na kuamua kufanya mambo yake kibiashara
zaidi, sasa kampuni yake kupitia matairi na betri za magari, inadhamini
timu tatu za Ligi Kuu Bara ambazo ni Mbeya City, Stand United na Ndanda
FC. Coastal wameanza kupitisha harambee kuweka mambo yao sawa!Simba kuna Kundi la Friends of Simba (FOS), linaundwa na wanachama wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara wakubwa, ni watu wazima wenye uwezo wa kifedha.
Ndiyo kundi linaloongoza kwa kujazwa kashfa karibu na kila anayekuwa madarakani au shabiki wa waliopo madarakani. Simba ikishinda FOS hawahusiki, ikifungwa wanakuwa wamehujumu wao.
Kumekuwa na kashfa nyingi kuhusiana na watu wa kundi hilo, lakini hakuna aliyewahi kusimama na kutoa ushahidi kuhusiana na wanaowatuhumu. Ikifika uchaguzi, hata kama hakuna mgombea anayetokea FOS, basi lazima utasikia kundi hilo limetajwa na lawama tele ambazo hazina uthibitisho.
Huenda wengi wanahofia kuzungumzia walichokifanya FOS kwenye maisha ya Simba, wanahofia kuonekana ‘wamenunuliwa’ kama ilivyozoeleka au kuwaudhi wale wasiowapenda FOS, mimi siogopi.
FOS wanaweza kuwa na mabaya yao, wao ni binadamu, lakini ni kundi lililofanya mazuri mengi Simba na yako wazi. Vipi kila kitu kwao ni matusi na lawama tu?
Wakikosea wakosolewe bila ya woga, huo ni msingi sahihi wa maendeleo, lakini walipopatia, ukweli uwe wazi na wasifiwe.
Kuna watu Simba ambao hawawapendi FOS lakini zitakuwa sababu binafsi na zaidi ni za kimaslahi, lakini huenda hata baadhi ya wapinzani wa Simba na hasa watani wao, Yanga, wasingependa kuwaona FOS wakiiongoza Simba, huenda wanakumbuka kile kipindi cha miaka saba bila kukishinda kikosi hicho kutoka Msimbazi.
Kwa miaka saba, Simba ikiwa na watu wengi wa FOS, iliinyanyasa Yanga ambayo ushindi wake dhidi yao ulikuwa ni sare, zaidi ya hapo ni kipigo. Hivyo, Yanga watakuwa na haki ya kutotaka kuwaona tena FOS wakirudi.
Mpira ni fedha, Azam FC inafanya mabadiliko sasa kwa kuwa ina fedha. Yanga kuna Yusuf Manji, uwezo wa mipango, uwezo wa kutoa mamilioni ya fedha, ndiyo maana wanachama walitaka abaki.
Unapoambiwa kuwa FOS wanainyonya Simba, halafu ukaangalia kundi hilo baadhi ya watu wake kama Crescentius Magori, Zacharia Hans Pope, Kassim Dewji, Mussa Batenga, Azim Dewji, Evans Aveva, Musley Al Rawah, Salim Try Again, Mohammed Nassor, Adam Mgoyi, Swed Nkwabi na wengine wengi ni watu wenye uwezo kifedha.
Kama wanaiibia Simba, jiulize Simba kwa mwaka inaingiza kiasi gani, inatumia kiasi gani na watu kama hao ambao wengine ni mamilionea, wanagawana kiasi gani ili wafaidike kama inavyoelezwa?
Simba inapokuwa imebanwa, hasa wakati wa mechi dhidi ya Yanga, hurudi na kuwaangukia ili waweke msaada wao, baada ya mafanikio hakuna kiongozi anayesema tena.
Wapo wanachama wanaosisitiza hivi: “Hata kama wanaiba, angalau wanatupa furaha ya ushindi.” Lakini katika wanaosema ni wezi, hakuna aliyewahi kuthibitisha au kutoa mfano zaidi ya mmoja kupokea maneno huku na kuyasambaza kule bila ya kuwa na uhakika.
Usajili:
Inawezekana kabisa kipindi hiki FOS watakuwa katika ushindani mkubwa katika suala la usajili, lakini inajulikana wakati ule walivyoitesa Yanga hasa ile chini ya Francis Kifukwe, walikuwa wakifanya wanavyotaka.
Simba ilikuwa na wachezaji karibu wote waliokuwa bora, taratibu walianzisha mpango wa kupata wachezaji bora na moja ya mifano mizuri ni pale mmoja wa wajumbe wao alipoamua kuuza basi na kumsajili Mark Sirengo kutoka Kenya.
Aveva ndiye alipewa kazi ya kusafiri hadi Nairobi kufanya mazungumzo na Sirengo, akafanikiwa kumleta nchini na alikuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa na wenye msaada mkubwa.
Kama unakumbuka akina Selemani Matola, Said Sued ‘Panucci’, Juma Kaseja, Christopher Alex, Boniface Pawasa, Ulimboka Mwakingwe, Victor Costa Nampoka na wengine ni wachezaji walioonekana kama hawafai mwanzo lakini nguvu ya FOS iliwarudisha na kuanza kujiamini, ubora wao ukaonekana.
Kukubalika:
Wapo wanaoamini FOS ni wababaishaji, waliopo kwa ajili ya kuivuruga Simba lakini kuna makocha wanasikia faraja na wanataka kufanya kazi na kundi hilo.
Mmoja wa makocha hao ni Patrick Phiri, raia wa Zambia, ambaye kila akiitwa Simba, basi lazima atauliza kama watu fulani wapo na wote ni memba wa FOS. Anaamini anaweza kufanya nao kazi vizuri na mambo yakaenda sawa.
Kocha mwingine ni Milovan Cirkovic raia wa Serbia, mmoja wa makocha vipenzi katika Klabu ya Simba ambaye aliondolewa nchini si kwa uwezo, badala yake kutokukubalika kwa baadhi ya viongozi wa Simba chini ya uongozi wa Ismail Rage, lakini pia baadhi ya wajumbe wa FOS ambao hayakuwa matakwa ya kundi hilo.
Kuondoka kwa Milovan ambaye aliiongoza Simba kutwaa ubingwa na kuitwanga Yanga kwa mabao 5-0, kipigo cha kihistoria, taratibu, kikosi kikaanza kuporomoka hadi kufikia kuonekana ni cha kawaida kama timu nyingi za kawaida.
Makosa:
FOS si malaika, kuna makosa mengi wamefanya kama binadamu na huenda mengine hatuyajui ingawa mafanikio na chachu yao katika soka ni changamoto.
Wakati mwingine wao kwa wao wamekuwa wakikinzana, wengine wanataka hili na wengine lile, maana wako wengi na asilimia kubwa wana uwezo kifedha.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha katika vipindi fulani Simba kuyumba kwa kuwa wao kwa wao hawaelewani. Hii imetokea mara kadhaa na hasa katika uamuzi wa masuala ya usajili wa wachezaji au kuajiri kocha mpya.
Inawezekana hata sasa kama Aveva ambaye ni mwenzao ataingia madarakani, basi makosa yakawepo kama binadamu. Lakini kama kweli ni wazoefu, wamepita kwingi basi wanapaswa kuwa watu waliojifunza na wasirudie makosa waliyopitia.
Badala yake wafanye kila wanachoamua kwa ajili ya Simba, ingawa kupishana kimawazo ni jambo la msingi sana. Kinachofikiwa katika uamuzi wa mwishoni vema kikaheshimiwa.
Katika kundi kubwa kama lao halikosi vikundi vingine vidogovidogo hata kama vitakuwa vimejificha ndani yake. Hivyo vinaweza kuwa hatari kwa FOS kwa kuchangia kufeli au hata kuivuruga Simba kabisa!
Faida:
Mmoja wa viongozi wa Friends of Simba, Kassim Dewji, ndiye aliyejenga jengo la pili la Simba ambalo linaiingizia klabu hiyo Sh milioni 180 kila mwezi, hakuna ambaye ameweza kusema ahsante.
Wengi wamekuwa wakisema msingi wake ulitakiwa kuwa wa ghorofa nane lakini umechakachuliwa, maana yake wanalaumiwa, lakini kila fedha zikiingia, zinatumika kuisaidia klabu na kuna uhakika wa nyingi tu zimekuwa zikiingia kwenye mifuko ya wajanja.
Mafanikio:
Simba wakati inafikia fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993, Azim Dewji ambaye sasa ni Friends of Simba, ndiye alikuwa mfadhili, Kassim Dewji alikuwa katibu mwenezi.
Mwaka 2003, Simba ikafanya jambo kubwa katika historia ya soka Afrika. Kwanza ikaifunga Zamalek kwa Cairo na kuivua ubingwa wa Afrika, hakuna timu ya Tanzania iliyowahi kufanya hivyo.
Pili, iliifunga na kuitoa mashindano timu bora kuliko zote barani Afrika katika kipindi hicho na kwa mara ya kwanza ikacheza hatua ya nane bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakati ikifanya mambo hayo, Simba ilikuwa chini ya uongozi wa katibu mkuu, Dewji ambaye ndiye aliongoza kila kitu kwa kushirikiana na FOS.
FOS ndiyo waliingia mifukoni na kuchangisha fedha ili kuongezea chache zilizokuwa zimepatikana kwa ajili ya kuweka kambi Oman.
Baadhi ya wajumbe wa FOS walitoa mamilioni kuhakikisha wanampata kocha Talib Hilal ambaye alikubali kupunguza bei na kusaidiana na kocha James Aggrey Siang’a, raia wa Kenya, kuinoa Simba ikiwa Oman kwa ajili ya mechi ya marudiano jijini Cairo.
Simba ilishinda na hadi leo imeweka rekodi nyingine ya kuwa timu iliyopokewa na watu wengi zaidi kuliko nyingine yoyote. Hiyo ilitokea wakati wakirejea kutoka Cairo na zaidi ya watu watatu walifariki dunia siku hiyo.
Zengwe:
FOS wanasifika kwa fitna za kisoka, wako wanaosema huwahonga marefa au wachezaji wa timu pinzani, lakini hakuna ambaye amewahi kuthibitisha.
Inabaki katika zile kauli zinazoelea za kwenye kahawa kama Manji kahonga au Azam FC imechukua ubingwa kwa kuwa ilihonga, vitu ambavyo vinakuwa havina ushahidi na vinalenga kuchafua tu.
Ingekuwa vizuri kama kuna mtu ana ushahidi na hilo na lengo lake ni zuri, basi angejitokeza na kuisaidia jamii yetu ya soka kuhusiana na kitu na ukweli uwe wazi kuhusu FOS badala ya taarifa za gizani, sawa na aliyefungua macho kwenye giza akijaribu kutembea huku anapapasa!
Inawezekana ndani ya FOS kuna watu wabaya, lakini haiwezekani wote wakawa wabaya. Vizuri kukawa na kipande cha kuwapa moyo kwa kuwa hali halisi inaonyesha wanajitolea.
FIN.
No comments:
Post a Comment