Wakati Kocha
mpya wa Simba, Patrick Phiri raia wa Zambia ametua nchini, angalia aliyekuwa
kocha wa timu hiyo, Zdravko Logarusic alivyoliaga jiji la Dar.
Kupitia mtandao
wa Facebook, Loga ametupia picha mbili huku akiandika “by by Tanzania),
akimaanisha bye bye Tanzania.
UONGOZI wa Simba umeamua kumfukuza kazi aliyekuwa kocha mkuu wa
timu hiyo, Zdravko Logarusic, lakini kocha huyo ameondoka na kitita cha
Sh56 milioni kwa muda wa wiki tatu pekee tangu aliposaini mkataba mpya
klabuni hapo bila kufanya kazi yoyote ya maana.
Logarusic amechukua kitita hicho akiwa ameiongoza
Simba kwenye mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya Zesco ya Zambia ndani ya
muda huo ambapo Simba ililala kwa mabao 3-0.
Kwanza Julai, 22 mwaka huu, kocha huyo alisaini
mkataba wa mwaka mmoja wa kukinoa kikosi hicho cha Simba ambapo
alichukua Dola 24, 000 (Sh 39.7 milioni) za ada ya kusaini mkataba huo.
Pili kocha huyo alipokea mshahara wa mwezi mmoja
aliofanya kazi ambao ulikuwa ukamilike wiki ijayo na pia amepokea
mshahara wa mwezi mmoja wa bure ili kuvunja mkataba wake.
Hivyo kocha huyo amepokea jumla ya dola 10,000 (Sh
16.5 milioni) za mishahara yake ya miezi miwili klabuni hapo. Jumla ya
fedha hizo ni Sh56milioni.
Mbali na fedha hizo alizoondoka nazo, kocha huyo
aliiongoza Simba kushika nafasi ya pili ya Kombe la Mapinduzi mapema
mwaka huu. Simba ilitinga fainali ya michuano hiyo ambapo ilipoteza kwa
bao 1-0 mbele ya KCCA ya Uganda.
Katika rekodi nyingine Logarusic aliiongoza Simba katika mechi 13 za Ligi Kuu Bara, Simba ilishinda mara tatu pekee.
Ilipoteza michezo mitano na kutoka sare mitano na
kumaliza nafasi ya nne. Logarusic aliikuta Simba katika nafasi hiyo hiyo
ya nne wakati anakabidhiwa timu Desemba mwaka jana kwa mkataba wa
kwanza.
No comments:
Post a Comment