Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema kuendelea vikao vya Bunge Maalumu la Katiba bila kuwapo maridhiano baina ya pande zinazovutana na upande mmoja ukibaki nje ya Bunge, ni sawa na kutumia vibaya fedha za Watanzania.
Amesema kauli kwamba akidi ya wajumbe wa Bunge
hilo imetimia na vikao vinaweza kuendelea haiwezi kuzaa Katiba
itakayokubaliwa na wananchi wote na ni tofauti na Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba inavyoeleza katika sehemu ya kufanya uamuzi.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wetu
ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema, “Kama uwezekano
wa kukutana upo, kwa nini Bunge liendelee kutumia fedha wakati mnajua
kuwa mwisho hamtafikia uamuzi? Jambo la msingi ni kujitahidi kuafikiana
na Bunge liwe na wajumbe wote.”
Kauli ya Warioba imeungwa mkono na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba wakati akichangia hoja ya mabadiliko ya kanuni ya Bunge hilo kwa kulitaka bunge hilo kujitathimini iwapo baada ya mjadala litaweza kufikia uamuzi, ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.
Akitoa hadhari hiyo bungeni jana, Nchemba ambaye
pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, alisema
ni vyema Bunge hilo likajiridhisha kuhusu namna linavyoweza kutumia siku
60 zilizowekwa kwa uhakika na umuhimu wa kuziondoa siku za Jumamosi
kitendo kinachosababisha kuongezeka hadi kufikia 84.
“Tujiridhishe na kukubali ukweli kwamba kukaa hapa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha rasimu hii haiwezi kueleweka kwa Watanzania. Ni lazima Watanzania watatuuliza tumefanya nini,” alisema.
Alisema kwa namna moja, ni vyema kujua idadi
halisi ya wale wanaoshiriki katika awamu ya pili ya Bunge hilo na wale
wasioshiriki, ili kutoa uthibitisho wa kihesabu kwamba uamuzi wa
kuendelea kwa bunge unaweza kuwa na maana.
Hata hivyo, Nchemba alisema ni vyema wakiendelea kujadili masuala muhimu na kwa kuwa wanakwenda kujadili sura muhimu zinazogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania, lakini kwa uhakika kwamba hatua hiyo itakuwa na manufaa kwa Watanzania katika hatua ya mwisho.
Alisisitiza kwamba iwapo hatua hiyo itashindikana,
utetezi wa mwisho hautaweza kueleweka kwa sababu suala la kutimia kwa
akidi kwa mujibu wa Katiba ni muhimu katika kufikia uamuzi na hasa
kuangalia upya umuhimu wa kufikia maridhiano kwa sasa.
Bunge la Katiba lilianza jana mjini Dodoma bila
kuwapo kwa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na
baadhi ya wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais waliosusa vikao hivyo.
Ukawa wanashinikiza kujadiliwa kwa rasimu ya
Katiba iliyotolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na si ile
iliyodai inaingizwa kinyemela na wajumbe wanaounga msimamo wa CCM wa
serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na rasimu.
Akizungumzia hali hiyo Jaji Warioba alisema: “Hatuwezi kupata
Katiba ambayo itakubaliwa na Watanzania bila makundi yote kukubaliana.
Ushauri wangu kwa makundi yanayovutana ni kufikia mwafaka na kwenda
bungeni kufanya kazi kwa pamoja.”
Alisema kitendo cha upande mmoja kuendelea na
vikao vya Bunge hilo bila upande mwingine kuwapo, hakina faida yoyote
kwa sababu mwishoni hawataweza kuchukua uamuzi wowote.
“Hawawezi kufanya uamuzi wowote kwa sababu Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba inaeleza kuwa ili uamuzi ufanyike ni lazima
iwepo theluthi mbili ya wajumbe kutoka kila upande wa muungano.
“Itakuwa na matatizo zaidi kama mkitunga Katiba na kuipitisha kwa idadi fulani ya watu na kuanza kupingwa wakati huohuo.”
Afafanua madai ya Lukuvi
Katika hatua nyingine, Jaji Joseph Warioba
alifafanua madai yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kuwa yeye (Warioba)
amewasilisha serikalini maoni mapya, ukiacha yale ambayo yapo katika
Rasimu ya Katiba.
Alisema maoni hayo aliyoyawasilisha serikalini
Machi 27, mwaka huu yalikuwa maoni yaliyotolewa na wananchi lakini
hayakuingizwa katika Rasimu kwa kuwa yanahusu tu Tanganyika, kwa kuwa
Rasimu iliyoandaliwa ilipendekeza serikali tatu na Zanzibar wana
utaratibu wao.
“Tuliona kuwa sura hizo hazifai kuwa katika Katiba
ya Jamhuri kwa sababu masuala hayo mawili; ardhi, Zanzibar wana sheria
na utaratibu wao, Tanzania Bara wana sheria na utaratibu wake” alisema
kama ilivyo wa Serikali za Mitaa.
CHANZO NI MWANANCHI
No comments:
Post a Comment