Zitto anasema kuwa hata vyama vichanga vinavyokua kama ACT-Tanzania na vingine, vina nafasi ya kuingia katika umoja huo ili kuzidisha nguvu ya upinzani kuing’oa CCM kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Mwanasiasa huyo, alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalum na gazeti hili, yaliyofanyika juzi nyumbani kwake jijini Dar es Salaam juu ya masuala mbali mbali ya kijamii na kisiasa, huku akieleza namna UKAWA wanavyoweza kufanikisha ushindi wa kuing’oa CCM.
Zitto alisema kuwa, uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Disemba 14 mwaka huu, uchukuliwe kama sehemu ya kujifunza makosa yatakayofanyiwa kazi kuelekea katika ushindi wa mwaka 2015.
“Nimefurahi kukutana na wenzangu wa CHADEMA wakati wa mashauriano juu ya maazimio ya kamati ya PAC, nimekulia CHADEMA…nimefanya kazi CHADEMA, wapo niliowalea kisiasa, wapo niliowapokea kina Silinde, Lyimo na wengine, hivyo kukutana nao kwa pamoja baada ya mtafuruku ulioanza Disemba 22 mwaka jana, kumenipa faraja sana na sioni shida kufanya kazi na UKAWA kwa maslahi ya nchi,”alisema Zitto.
Alisema tofauti yake na chama chake haiwezi kumzuia kufanya kazi na UKAWA na kwamba hata kukutana kwao katika kujadili maazimio ya kamati ya Bunge kwa ajili ya kuwachukulia hatua watuhumiwa wa kashfa ya Escrow, ulikuwa mpango wa Mungu.
Kwa mujibu wa Zitto, ili UKAWA waweze kushinda katika uchaguzi ujao ni vema viongozi pasipo kujali maslahi binafsi, wakajiwekea malengo ya idadi ya viti vya ubunge watakavyopigania kwa nguvu zote wakiwa katika mgawanyo watakaokubaliana.
“Katika hili la ushindi kwa upinzani ndani ya muunagano ni dhahiri hauna mjadala, cha muhimu ni kukubaliana kwa mfano kuwa wanataka wabunge wangapi watakaowapigania kwa pamoja na hapa wasipungue 150 kwa mgawanyo utakaokubalika; mfano Zanzibar, CUF wasimamishe wagombea katika majimbo yote na bara wapate katika baadhi ya maeneo wanayokubalika,” alisema na kuongeza;
“CHADEMA NCCR-Mageuzi na ACT-Tanzania waweke wagombea kwa upande wa bara katika maeneo wanayokubalika na kila mgombea apiganiwe kwa nguvu zote katika eneo analokubalika dhidi ya mgombea wa CCM,”alisema Zitto.
Alisema vyama hivyo kwa umoja wao vikiwa na uhakika wa kupata wabunge 150, wasiokuwa na ushindani kutoka CCM, wanaweza kugombania majimbo mengine kwa ajili ya kuongeza idadi ya wabunge kwa lengo la kupata serikali yenye nguvu zaidi.
Kuhusu kutafuta maridhiano ndani ya CHADEMA, Zitto alisema maridhiano ya aina yoyote yatakayofanywa yanapaswa kuwashirikisha watu wote walioumizwa na shutuma alizopewa.
“Nimesamehe kila aina ya matusi niliyofanyiwa lakini mambo mawili sitoweza kuyaacha, moja ni kutaka shutuma kuwa ninatumiwa na CCM kwa ajili ya usaliti ithibitishwe na kama haupo waliotunga uongo huo wawajibishwe kwa kuwa hii pasipo kuthibitishwa kwa tuhuma hizo za usaliti, kutamuathiri hata mwanangu na kizazi change,”alisema Zitto.
Alisema yupo tayari kuwajibika kwa yale atakayoyafanya kuliko kuvumilia baadhi ya mambo yasiyokuwa na maslahi kwa Umma.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment