Mkali katika tasnia ya filamu Bongo, Eshe Buheti.
Kama ilivyo ada naye aliwekwa mtukati na mwandishi wetu Imelda Mtema
na kuulizwa maswali ambayo alitoa ushirikiano katika kuyajibu.Ijumaa:
Unaonekana kutoandamwa na skendo kama inavyokuwa kwa mastaa wengine, hii
inatokana na nini?Eshe: Unajua mimi ni mke wa mtu, najichunga sana kuhakikisha sichafuki kwa namna yoyote, ndiyo maana unaona skendo zinanipitia mbali.
Ijumaa: Hebu tuambie, unapokuwa nyumbani unapendelea kuvaa mavazi gani?
Eshe: Nikiwa ndani kwangu hasa na mume wangu akiwepo ni mwendo wa khanga moja kwa kwenda mbele.
Ijumaa: Mastaa mbalimbali inakuwa vigumu kuolewa na wakiolewa hawadumu kwenye ndoa zao, wewe unadhani utadumu?
Eshe: Kila jambo anapanga Mungu, kikubwa najitahidi kumheshimu mume wangu na kumfanyia kila linalomfurahisha na kuacha yanayomkera, naamini kwa kufanya hivyo ndoa yetu itadumu.
Ijumaa: Najua una mtoto mmoja sasa, vipi una mpango wa kuongeza mwingine soon?
Eshe: Mwanangu anaonesha kabisa anataka mdogo wake, kwa hiyo tunajipanga na naamimi hatuna muda mrefu tutafanya maandalizi ya kumleta kiumbe mwingine duniani.
Ijumaa: Wanaume wengi hawapendi kazi ya usanii hasa kutokana na skendo mbalimbali, vipi wewe mume wako amewezaje kukubaliana na kazi yako?
Eshe: Nahisi mume wangu ni mtu wa tofauti, ananiamini na kwa kuwa hajawahi kusikia lolote baya, wala hana wasiwasi.
Ijumaa: Kuna mastaa ambao wana katabia ka’ kuiba waume za watu, siku ukijua kuna anayemnyemelea mumeo utafanyaje?
Eshe: Huyo atakuwa ananitafuta shari na kwa kweli ajiandae kwa mpambano. Siwezi kuingiliwa kwenye anga zangu halafu nione sawa tu.
Ijumaa: Kutokana na tabia ya mastaa wengi kuwa na kucha ndefu na kutopenda kiziharibu hata kupika hawawezi, wewe kwako hili likoje?
Eshe: Kwa mambo ya mahanjumati yani hapa ndiyo umefika, omba siku nikualike uje kula kwangu ndiyo utajua mimi ni mpishi au mbabaishaji.
Ijumaa: Ni mambo gani ambayo huyapendi kabisa kwenye maisha yako?
Eshe: Mimi sipendi umbeya, uvivu, majungu kwani ni vitu ambavyo vinaturudisha nyuma.
Ijumaa: Kwenye sanaa kuna vishawishi vingi sana hasa hii tabia ya baadhi ya maprodyuza kupenda sana rushwa ya ngono, wewe unakabiliana vipi na changamoto hiyo?
Eshe: Najitambua na ninajiheshimu sana. Siwezi kujivunjia heshima yangu kwa mambo ya kijinga kwa hiyo Mungu ananisaidia navuka changamoto hizo.
Ijumaa: Unawashauri vipi hawa mastaa ambao mabifu ni sehemu ya maisha yao?
Eshe: Hili ni tatizo na kwa kweli ni vyema sisi mastaa tukawa na umoja na tukashirikiana katika kuendeleza sanaa yetu badala ya kugombana.
No comments:
Post a Comment