CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS
YULE mahabusu aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwenye uzio wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Desemba 31, mwaka huu jijini Dar ni huyu ambaye anaonekana sura vizuri ukurasa wa kwanza wa gazeti hili.
Anaitwa Abdul Koroma ni raia wa Siera Leone. Mpaka siku ya kifo chake alikuwa na miaka 33. Koroma aliuawa na askari magereza akijaribu kutoroka kesi ya madai ya kukutwa na madawa ya kulevya aina ya cocaine.
ALIKUWA ASKARI MUASI
Baada ya kifo chake, Uwazi kama kawaida yake lilifuatilia kwa karibu ili kujua nini ni nini kwa marehemu huyo ambaye jina lake na la ukoo linafanana na rais wa nchi yake, (Abdul Koroma).
Marehemu Koroma alikuwa muasi wa jeshi la nchi yake na aliwahi kujiunga na Kundi la uasi la Sedeka ambalo liliweka ngome yake nchini Afrika ya Kati.
Baada ya kundi hilo kusambaratishwa, Koroma alikimbilia nchini Uingereza ambako alipata kazi ya kutunza wazee kwenye kituo cha kuwalea.
ALIOA MKENYA
Taarifa zaidi zinasema, marehemu akiwa Uingereza alikutana na Mkenya aliyejulikana kwa jina la Debora Wangui ambapo walifunga ndoa lakini maisha yakawa magumu, hivyo Koroma akaamua kujiunga na mtandao wa biashara haramu ya usafirishaji wa madawa ya kulevya.
...Baada ya kukamatwa na unga.
MAHAKAMANI KISUTUTaarifa zaidi zinasema, marehemu akiwa Uingereza alikutana na Mkenya aliyejulikana kwa jina la Debora Wangui ambapo walifunga ndoa lakini maisha yakawa magumu, hivyo Koroma akaamua kujiunga na mtandao wa biashara haramu ya usafirishaji wa madawa ya kulevya.
...Baada ya kukamatwa na unga.
Uwazi lilifika eneo la tukio kwa ndani na nje ya uzio wa Mahakama ya Kisutu na kubaini kuwa, utorokaji wa Koroma siku hiyo haukuwa uamuzi wake bali ni mpango uliosukwa na mtandao wa baadhi ya wauza unga wa jijini Dar es Salaam.
“Ndiyo maana aliweza kukutwa na karatasi ya ramani kwenye mfuko wa suruali,” kilisema chanzo chetu cha habari.
BODABODA ZILIMSUBIRI NJE YA UZIO
Nao mashuhuda waliohojiwa na Uwazi nje ya uzio wa Mahakama ya Kisutu siku ya tukio, eneo alilouawa Koroma walisema kulikuwa na bodaboda mbili nyekundu nje. Moja ilikuwa na watu wawili, nyingine ilikuwa na mtu mmoja.
“Wote walivaa majaketi. Baada ya yule askari magereza kufyatua risasi mbii hewani, baadaye akampiga nayo moja jamaa, wenye bodaboda walionekana kuchanganyikiwa na kuondoka kwa kasi. “Inaonesha walikuwa wamepanga wamtoroshe. Kama angefanikiwa kuruka uzio angepanda bodaboda moja,” alisema shuhuda mmoja kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Mashuhuda hao walisema kuwa, baadhi ya watu waliokuwa wakipita eneo hilo waliwauliza bodaboda hao kama wanachukua abiria wakawa wanakataa.
“Awali tulidhani ni majambazi lakini baada ya tukio tukabaini kwamba wale walikuwa kundi moja na marehemu,” alisema shuhuda mwingine.
KAMA KOROMA ANGETOROKA
Taarifa zaidi zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya maofisa wa usalama zilidai kwamba, bodaboda hao ni mtandao wa marehemu na walikuwa pale ili kama mtuhumiwa huyo angefanikiwa kutoroka kwa kuruka uzio, wangemchukua na kutokomea naye kusikojulikana na baadaye usiku angesafirishwa nje ya nchi.
UWAZI LATUA GEREZA LA KEKO
Vyanzo vyetu makini ndani ya Gereza la Keko jijini Dar vinasema kwamba, Koroma alikuwa mtu hatari katika gereza hilo kwani alikuwa na tabia ya kikatili.
“Hapa gerezani alikuwa akiwapiga na kuwatesa mahabusu wenzake. Mara kwa mara alikuwa akionywa na askari lakini alikuwa mkaidi kutii maagizo ya askari.
“Wapelelezi wa gereza walifuatilia nyendo zake kwa kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) wakagundua kuwa, Koroma alikuwa amepitia mafunzo mbalimbali ya kijeshi.”
KWA NINI ALIPIGWA RISASI?
“Sisi askari wa gereza tulikuwa makini naye baada ya kupokea taarifa hizo na ndiyo maana tulipomwona anatoroka mahakamani Kisutu tulijua hatuwezi kumpata tena.
“Hali ile ilisababisha apigwe risasi kwani uzembe wowote ungeweza kumfanya amnyang’anye bunduki askari na angeweza kuleta maafa pale.
“Na nataka jamii ujue kuwa, Koroma kama ngetoroka ingekuwa sifa mbaya kwa askari waliokuwepo mahakamani kwani ingetafsiriwa kuwa kuna njama na mtandao wa wauza madawa ya kulevya,” kilimaliza kusema chanzo chetu.
MKUU WA GEREZA LA KEKO
Mkuu wa Gereza la Keko, Kamishina Msaidizi wa Magereza, ACP Mbwana Senashida alililiambia gazeti hili kwa njia ya simu ya kiganjani kuwa, maisha ya Koroma ndani ya gereza hilo yalikuwa ya hatari.
“Alikuwa mtu hatari kwani hata ndani ya mahabusu alikuwa akifanya mazoezi, kupiga mahabusu wenzake na alipokuwa akikatazwa alikuwa anatii kwa muda na kuanza tena vurugu baada ya muda mfupi.”
ALIZOEA KUISHI MSITUNI
“Hawa watu walikuwa wakiishi msituni kwa muda mrefu huko kwao, hivyo kuishi na jamii kama hapa ndani ya gereza si jambo la kawaida,” alisema.
Aliongeza kuwa, Koroma alifikishwa katika gereza hilo, Desemba 2013 baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya na kuishi Tanzania kinyume na sheria.
Kuhusu askari aliyempiga risasi marehemu, mkuu huyo alisema uchunguzi unaendelea.
ALIVYOKAMATWA NA UNGA
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Godfrey Nzowa alipoulizwa na mwandishi wetu ofisini kwake juzi kuhusu Koroma, alisema:
“Koroma tulimkamata Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Desemba mbili, 2013 mchana. Alikuwa akitokea Brazili akiwa na pipi 95 za cocaine zenye thamani ya shilingi milioni 61.”
No comments:
Post a Comment