Mpenzi msomaji wangu, ukijaribu kutafuta maana halisi ya mapenzi utapata tafsiri nyingi sana lakini kwa ninavyojua mimi, mapenzi ni hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine.
Hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na za dhati huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo.
Hii ndiyo maana ya harakaharaka ya mapenzi. Najua na wewe unaweza kuwa na tafsiri yako lakini leo tusimamie kwenye hii ili niweze kukufikishia kile nilichodhamiria.
Ukweli ni kwamba, unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu uliyetokea kumpenda sana hupaswi kuwa na mtu mwingine kwa kuwa, kufanya hivyo utakuwa unaunyima haki moyo wako.Ndiyo maana kila siku tunasisitizwa kuwa waaminifu na kuridhika na mapenzi kutoka kwa wale tunaowapenda. Hata hivyo, hali sasa hivi imebadilika, maana ya mapenzi imepotoshwa kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba sasa umebaki usanii tu.
Leo hii unaweza kumpenda mtu f’lani, ukawa hulali, huli wala kufanya kazi zako vizuri kutokana na unavyomfikiria huyo uliyetokea kumpenda. Hiyo ni hali ya kawaida kwenye mapenzi.Hata hivyo, wewe unaweza kuwa katika hali hiyo lakini cha ajabu huyo unayempenda wala hana taimu na wewe na unaweza kujitahidi kufikisha hisia zako na zikapuuzwa.
Hapo ndipo baadhi wanapofikia hatua ya kuchanganyikiwa na kuhisi hawana thamani. Wanajihisi hivyo kwa kuwa penzi lao halithaminiwi.Nadhani katika hili kuna kitu tunakosea. Hivi unadhani kila utakayetokea kumpenda naye lazima akupende na akubali kuwa na wewe? Ni wangapi ambao huenda wameshawahi kukutokea na kukueleza kuwa wanakupenda sana lakini wewe mwenyewe huna hata chembe ya mapenzi juu yao?
Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba, asilimia kubwa wapo kwenye uhusiano na watu wasiowapenda. Hii ni kwa sababu ni nadra sana kumpenda mtu na yeye akawa anakupenda kama unavyompenda wewe.
Jaribu kufuatilia utagundua kwamba ndoa nyingi zinayumba na nyingine zinavunjika kwa kuwa, mmoja hana mapenzi ya kweli kwa mwingine. Wapenzi nao wengi wao wanaishi ili mradi siku zinakwenda na ikitokea wameachana kuna mmoja kati yao atachukulia poa na mwingine ataumia kwa kuwa alipenda zaidi.
Kwa maana hiyo basi ukae ukijua kwamba, kumpenda mtu kisha yeye akawa haoneshi kukupenda wala siyo tatizo, tatizo litakuja tu pale ambapo wewe utakuwa hujagundua kuwa hupendwi. Kwa bahati ukimpenda mtu kisha Mungu akakujaalia ukagundua kuwa yeye hakupendi, chukulia kuwa hiyo ni hali ya kawaida na uamuzi sahihi ni kuamua kuachana naye.
Kosa kubwa ambalo utalifanya ni kung’ang’ania kumpenda mtu ambaye anaonekana kutokuwa na mapenzi na wewe. Kwa nini umuendee mtu kwa mganga eti ili akupende? Hivi unadhani yeye ndiyo yeye na hakuna mwingine wa kuwa na wewe?
Acha umbulula, una kila sababu ya kuhakikisha unajiweka katika mikono salama. Ikiwa umempenda mtu kisha unapomueleza hisia zako haoneshi kujali, mtoe katika moyo wako.
Kumbuka ukiendelea kumsumbua, itafika wakati ataona akukubalie tu akijua atakupelekapeleka, atakutumia na mwisho atakuacha. Ni wangapi ambao unawajua sasa hivi wanalia kwa sababu wamelazimisha mapenzi? Ni wengi sana huko mtaani hivyo ni vyema wewe ukajitoa kwenye kundi hilo.
No comments:
Post a Comment