Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka
Pia wamesema kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amelidanganya Bunge kwa kusema kuwa madai ya madaktari tayari yameshashughulikiwa wakati siyo kweli.
Akitangaza kuanza kwa mgomo huo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, alisema hadi sasa hakuna makubaliano yoyote yaliyofanyika kuhusiana na madai ya madaktari.
Alisema wameshindwa kuelewa ni kwa nini serikali imeshindwa kugusia hoja za msingi waliyoitoa ya kutaka huduma za hospitali ziboreshwe, ikiwemo kuongeza dawa, mashine na vitendea kazi ili wagonjwa wapatiwe matibabu yenye ubora.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa serikali haijalikugusia suala hilo, hali inayosababishia huduma kuwa duni.
“Tumeamua kutangaza mgomo rasmi kuanza Jumamosi (kesho) na hautakuwa na kikomo, serikali inadanganya kuwa imetekeleza madai yetu, jambo ambalo siyo la kweli, hakuna makubaliano yoyote,” alisema.
Dk. Ulimboka alisema wananchi wanatakiwa kuelewa kuwa wanachokipigania madaktari ni kubadili hali ya huduma ambayo imekuwa mbaya katika hospitali na kusababisha wagonjwa kufariki kutokana na kupatiwa huduma katika mazingira magumu.
Alisema ufumbuzi utapatikana pale serikali itakapokuwa tayari kutatua madai yao na siyo vinginevyo kwani jambo hilo linachukuliwa kisiasa zaidi.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk. Edwin Chitage, alisema kuwa kuna upotoshwaji katika taarifa ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussen Mwinyi.
Alisema katika madai matano ambayo Dk. Mwinyi ameeleza kuwa wameafikiana hakuna ukweli.
Akitolea ufafanuzi juu ya suala hilo, alisema nyongeza ya posho ya kuitwa kazini haitapanda kama walivyoahidiwa na Pinda kwamba ingeongezwa katika bajeti ya mwaka 2012/2013 kutoka Sh. 10,000 - 25,000 hadi Sh. 40,000 - 50,000.
Alisema nyongeza hiyo imefutwa katika meza ya majadiliano kati ya serikali na madaktari.
Dk. Chitage alisema serikali imewaongezea posho ya uchunguzi wa maiti kutoka Sh. 10,000 hadi Sh. 100,000 ingawa hawajawahi kuwasilisha dai hilo.
Alieleza kuwa katika suala la kadi ya bima bado hawajakubaliana kwani wamepewa taarifa kuwa suala hilo linaendelea kujadiliwa na Mfuko wa Bima ya Afya, hivyo suala halijatekelezwa kama serikali inavyodai.
Akizungumzia suala la chanjo kwa madaktari, Dk. Chitage alisema kuwa serikali imewaeleza itawapatia chanjo hiyo kwa awamu na kwamba suala hilo hawajafikia makubaliano.
Alisema suala la kuwajibishwa kwa viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii haikuwa hoja ya kamati kwani lilikuwa linashughulikiwa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Waziri Mkuu Pinda.
Dk. Chitage alisema suala la posho ya nyumba limetolewa na kamati hiyo licha ya kwamba tayari Waziri Mkuu alishaahidi kulishughulikia.
Kuhusu nyongeza ya mshahara, alisema kiwango hicho cha Sh. milioni 3.5 walikichagua kuendana na mazingira yao ya kazi na kwamba serikali ilitakiwa iwajulishe itatekeleza kwa kiasi gani na siyo kueleza kuwa suala hilo haliwezi kutekelezeka.
Alisema waliamua kuchagua kiasi hicho kiwe kima cha chini kwa mshahara wa madaktari na kwamba serikali ilitakiwa kukaa meza moja na kujadiliana nao ili iwaeleza kiasi ambacho ina uwezo wa kuwalipa.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk. Godbless Charles, alisema kuwa hoja zao ambazo waliziwasiliza kwa Waziri Mkuu mpaka sasa hazijafanyiwa kazi.
Alisema kutokana na hali hiyo, imewabidi waazimie kutangaza mgomo kwa kuwa serikali haina nia ya kutekeleza madai yao.
Juni mwaka huu madaktari waliipa serikali wiki mbili kuhakikisha inatekeleza madai yao, vinginevyo watagoma kama walivyogoma Januari na Februari mwaka huu uliotikisa sekta ya afya na kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa katika hospitali nyingi za umma. Wiki mbili zinaisha leo.
KAULI YA PINDA BUNGENI JANA
Akijibu swali bungeni jana, Pinda alisema mgogoro kati ya madaktari na serikali umefikishwa katika Tume ya Usuluhishi na Upatanishi (CMA), baada ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kushindwa kufikia mwafaka kuhusu madai matano ya madaktari.
Alikuwa akijibu swali la papo kwa hapo lililoulizwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliyetaka kujua kama serikali imekwishafanya mazungumza na madaktari kufuatia mgororo huo.
Katika swali lake, Mbowe alitaka kujua ni mambo gani ambayo serikali walikubaliana na madaktari na yapi ambayo hawajakubaliana.
Pinda alisema serikali ilikuwa na mgogoro na madaktari na kwamba wamekuwa wakizungumza nao na kwa mwezi mmoja sasa. Alisema timu iliyoundwa kati ya madaktari na serikali ilimaliza kazi yake na walifikia makubaliano ya mambo matano.
Pinda alisema kuwa walikubalina kuhusu posho ya uchunguzi wa maiti kuwa Sh. 100,000 kwa daktari bingwa na msaidizi wake Sh. 50,000; pia walikubaliana juu ya posho ya kuitwa kazini kwa dharura.
Lakini alisema timu hiyo haikukubaliana katika mambo mengine matano kama posho za usafiri, nyumba, mazingira magumu ya kazi, na nyongeza ya mshahara, hivyo serikali iliona lifikishwe Mahakama ya Usuluhishi (CMA).
DODOMA WAUNGA MKONO MGOMO
Jumuiya ya Madaktari na Wahudumu wa Afya mkoani Dodoma imetangaza mgogoro na serikali na kwamba wako tayari kuungana na wenzao kugoma kesho.
Mwenyekiti wa Jumuiya wa madaktari mkoani Dodoma, Dk. Kassian Mkuwa, alitoa msimamo huo jana katika kikao cha madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Dk. Mkuwa alisema hatua hiyo ni kuunga mkono maamuzi ya kikao cha madaktari na wahudumu wa afya kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi huu kilichoukataa ufafanuzi uliotolewa na serikali juu ya madai yao ya msingi.
Alisema ufafanuzi huo wa serikali hauna nia ya dhati ya kuleta suluhisho la kudumu katika sekta ya afya.
Aliongeza kuwa wanaitaka serikali iache mara moja jitihada zake za kuwagawa wahudumu wa sekta ya afya kwani kwa kuwa kufanya hivyo kutazorotesha ufanisi wa utoaji wa huduma za afya nchini.
Hata hivyo, aliitaka serikali kuwalipa mara moja watumishi wa afya posho mpya za kuitwa kazini.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya hiyo, Gustavos Deusdedith, alisema: “Tatizo ni kuwa serikali imekuwa ikitufanya sisi kama watoto, kwa maana hiyo imeshishindwa kutekeleza makubaliano kama walivyotuahidi katika madai yetu.”
“Walichofanya serikali katika madai yetu ni kuongeza posho ya madaktari wanaofanya uchunguzi wa maiti kutoka Sh. 10,000 hadi Sh.100,000 wakati madaktari wenyewe hawazidi 10, sijui ndiyo njia ya kutatua madai yetu?” alihoji.
Alisema ukimya huo wa serikali utawafanya kuungana na madaktari wengine kwenye mgomo wa nchi nzima kuanzia kesho kutokana na kutoridhishwa na majibu ya serikali kwenye madai mbalimbali.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk. Emmanuel Mpuya, alisema hana taarifa za madaktari hao kugoma, bali anachofahamu kwa sasa ni kuwa wako katika majadiliano na serikali.
Dk. Mpuya alisema haungi mkono mgomo huo kwa kuwa unaweza kuwaumiza wananchi wasio na uwezo.
Madaktari wa Hospitali za Rufani za Bugando ya mkoani Mwanza na KCMC wamekwisha kutoa taarifa ya kuunga mkono mgomo huo.
Imeandikwa na Beatrice Shayo, Dar; John Ngunge na Peter Mkwavila, Dodoma.
CHANZO: GAZETI LA NIPASHE LA 22/6/2012
No comments:
Post a Comment