HUKU kukiwa na juhudi za kutambuliwa na kuthaminiwa kazi za
wasanii ndani na nje ya nchi, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),
limewataka wasanii kuongeza thamani kwenye kazi zao ili kuzipa ubora
zaidi.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,
Mafunzo na Habari wa BASATA, Godfrey Lebejo, wakati akihitimisha
programu maalumu iliyohusu Ubunifu, Utengenezaji na Uongezaji thamani
katika kazi za sanaa kupitia Jukwaa la Sanaa.
Alisema kuwa, ubora katika sanaa, unapatikana pia kwa wasanii
kuangalia wenzao wanafanya nini na wao kupata ubunifu mpya kwa kuongeza
vionjo, uthamani na ubunifu binafsi katika kuifanya kazi ya sanaa kwanza
kupendwa na baadaye kupewa thamani kubwa sokoni.
“Ni wazi wasanii wetu wanapaswa kuzingatia uongezaji uthamani kwenye
kazi wanazozifanya. Kubuni kazi ni suala moja lakini kuongeza uthamani
katika kazi yako ili ivutie wengi na kuuzika kwa thamani kubwa ni suala
lingine la kuzingatia” alisistiza Lebejo.
Aliongeza kuwa, kwa sasa kuna taarifa za Wakenya, kununua kazi za
wasanii wa Tanzania kwa bei ya chini na baadaye kuziongezea ubunifu,
thamani na kuziuza nje kwa bei kubwa.
Katika hilo, anasema, inatokana na wasanii wa hapa nchini
kutokuzingatia falsafa hiyo ya ubunifu na uongezaji thamani wa kazi zao.
Awali akiendesha darasa hilo maalumu, ambalo wiki hii lilikuwa mahsusi
kwa ajili ya wasanii na wajasiriamali wa sanaa za mikono (Handcrafts),
Haroun Sabili kutoka asasi ya Musoma Handcraft alisema kuwa, sanaa hizo
zinahitaji ubunifu na umakini mkubwa, kwani kinyume chake ni kutokuvutia
na kupoteza uthamani.
Alitoa wito kwa wasanii, kujiunga katika vikundi na kuwa rasmi ili
kuhakikisha, kwanza wanajenga mazingira ya kuwezeshwa, lakini pia kupata
mafunzo mbalimbali ambayo yatawafanya wazalishe kazi zenye ubora na
thamani kubwa.
Katika programu hiyo iliyohudhuriwa na wadau 72, elimu kuhusu ubunifu
na uongezaji thamani kwenye kazi za sanaa ilitolewa, sambamba na
malighafi mbalimbali na jinsi zinavyoweza kutumika kuzalisha kazi za
mikono kuoneshwa.
No comments:
Post a Comment