MGOMBEA nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi mdogo wa klabu ya
Yanga utakaofanyika Julai 15, Yusuf Manji, amesema haendi Jangwani
kutafuta fedha wala umaarufu, akisema hana njaa ya vitu hivyo.
Akizungumza Manji aliyetua
Yanga mara ya kwanza Juni, 2006 kupitia ufadhili, alisema anakwenda
Jangwani kurejesha furaha iliyotoweka.
Manji amesema, baada ya kuwa kwake ndani ya klabu hiyo kwa miaka sita,
kama mfadhili, mwanachama na mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, amejionea na
kujifunza mengi, hivyo anajua wapi pa kuanzia.
Alisema ingawa klabu hiyo inapaswa kujengewa msingi imara wa kiuchumi, lakini zawadi na faraja kubwa kwa wanachama, wapenzi
na mashabiki, ni mafanikio ya uwanjani kwanza.
“Najua wengi watakuwa wamejiuliza maswali mengi, iweje nichukue fomu,
kwanini nisibaki kuwa mfadhili, ninakwenda kutafuta nini, lakini
si kingine, ni kuwapa Yanga furaha,” alisema Manji kwa kujiamini.
Alisema amechukua uamuzi huo mgumu baada ya kubaini hakuna
njia nyingine ya kufanikisha ndoto zake za kuijenga Yanga imara kisoka
na kiuchumi, isipokuwa kuingia kwenye uongozi kuonesha njia.
“Nimechukua fomu nikitaka kutimiza ndoto za kuifanya Yanga ya mfano
Tanzania na Afrika kama nitapewa kura, pia sapoti baada ya kuingia
madarakani nikishirikiana na wenzangu,” alisema na kuongeza:
“Nikiwa mfadhili, kuna mambo niliyapigania kwa maslahi ya Yanga
bila mafanikio, nikaamua kujivua ufadhili (2009) na ujumbe wa Bodi
ya Udhamini (Februari, 2011), nikibaki mwanachama tu,” alisisitiza.
Manji alisema, baada ya mambo kwenda hovyo ndani ya klabu hiyo
hivi karibuni, wazee na vijana walimfuata wakimsihi arejee kwenye
ufadhili, lakini akaona hilo pekee halitoshi, yatakuwa yaleyale.
Alisema, kiu ya kuwania uongozi kwa kiasi kikubwa imechagizwa
na mapenzi yake makubwa kwa Yanga, hasa baada ya kuvuliwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kufungwa 5-0 na Simba katika mechi
ya kufunga pazia, Mei 6.
Alisema, vitu hivyo vimewanyima raha wanachama (akiwemo yeye), wapenzi
na mashabiki wa soka, hivyo anaomba kura za wenzake akiwa na agenda
nyingi; kubwa zaidi kurejesha furaha ya ushindi Jangwani.
Alisema, hiyo ni agenda muhimu zaidi kwa sababu, bila timu kufanya
vizuri dimbani, hata mipango ya maendeleo ikiwamo uwekezaji,
haitapangika, hivyo agenda yake ya kwanza ni kujenga kikosi imara cha
mataji.
Manji alisema, hilo haliwezi kufanikiwa kwa maneno, bali kwa vitendo
ikiwamo uwekezaji wa uhakika katika kikosi cha kwanza; kusajili nyota
bora na kuwalipa vizuri tena kwa wakati, pia kuwa na kocha bora.
Alisema, baada ya kurejesha furaha kupitia ushindi, ndipo amani,
utulivu na mshikanao vitakapotuama Yanga, hivyo uongozi kuanza kufikiria
mipango zaidi ya maendeleo ikiwamo uwekezaji.
Alisema chini ya mazingira hayo Yanga haiwezi kufungwa 5-0 v
na ikitokea hivyo tena chini ya uongozi wake, hatasubiri shinikizo v
la wanachama kumng’oa, atajiweka kando mara moja.
Mbali ya Manji, wagombea wengine wa nafasi hiyo katika uchaguzi huo
mdogo utakaofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es
Salaam, ni Sarah Ramadhan, John Jembele na Edger Chibula.
Uchaguzi huo unafanyika kujaza nafasi sita zilizo wazi baada ya
kujiuzulu kwa waliokuwa wakizishikilia kwa nyakati na sababu tofauti,
hivyo uongozi huo uliochaguliwa Julai 18, 2010 kusaliwa na wajumbe wanne
tu.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment