WATU 15 wa familia ya Mzee Ryoba Isiaga wa Kijiji cha Nkongore,
wilayani Tarime mkoani Mara, wamekosa chakula na mahali pa kuishi baada
ya kuchomewa nyumba nne, maghala ya nafaka na vitu vingine vilivyokuwamo
ndani.
Kwa mujibu wa Isiaga, walivamiwa na watu sita ambao walishindwa
kupambana nao hivyo walikimbilia ndani ya nyumba zao kujisalimisha,
lakini wakajikuta wakifungiwa kwa nje kisha kukawashwa moto ili waungue
wakiwa ndani.
Wavamizi hao waliosababisha hasara ya sh milioni 5 wanadaiwa walikuwa sita na wapo jirani na familia hiyo.
“Tulikimbizwa na vijana hao sita, na vijana wangu watatu baada ya
kushindwa kupambana nao kisha kuingia ndani… nyumba zilizochomwa moto,
wakati tupo ndani.
“Watu hao waliwasha nyumba zote nne moto na maghala matatu ya nafaka,
tulijiokoa baada ya kufanya nguvu hadi kumjeruhi mmoja wao ndipo
tulitoka nje na kupiga yowe… watu hao waliua ng’ombe mmoja kwa kumkata
na panga aliyekuwa amefungwa kwa kula nyasi,” alisema Isiaga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkongore William Matiko alisema alifika
kwenye tukio hilo baada ya kupatiwa taarifa na kushuhudia nyumba nne za
nyasi zikiwa zimeunguzwa na maghala matatu ya vyakula vya nafaka na
kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa ndani.
Matiko alisema alichukua hatua ya kulijulisha Jeshi la Polisi ambapo
walifika katika eneo hilo na kuchukua taarifa zake muda huo wakati
waliohusika na tukio hilo wakiwa wamekimbia kusikojulikana na kuacha
familia hizo zikiteseka bila kupata chakula na mahali pa kulala.
Familia hizo zinakusudia kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John
Henjewele kwa lengo la kupatiwa msaada wa chakula kutoka katika Mfuko wa
Maafa na mahali pa kuishi.
No comments:
Post a Comment