WAKATI shinikizo la baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kutaka
kususia sensa likishika kasi, serikali imewaomba radhi Waislamu
kutokana na matangazo yaliyorushwa na Kituo cha Televisheni ya Taifa
(TBC), yaliyoonesha kwamba idadi ya Wakristo nchini ni kubwa kuliko
Waislamu.
TBC ilirusha matangazo hayo siku ya Sikukuu ya Muungano (Aprili 26)
mwaka huu na kuonesha idadi ya Wakristo ni asilimia 52, Waislamu
asilimia 32 na madhehebu mengine asilimia 14.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari
(Maelezo) jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa TBC, Clement Mshana
alisema kuwa matangazo hayo yalitolewa kwenye mtandao wa
Wikipedia na
kurushwa hewani kimakosa.
Alisema baada ya kurushwa kwa matangazo hayo kimakosa, TBC walipokea
barua nyingi kutoka Chama cha Wanataaluma wa Kiislamu Tanzania (Tanzania
Muslim Professional Association) zikieleza kukerwa na taarifa hiyo.
Mshana Alisema katika barua hiyo, chama hicho kilitaka ufafanuzi jinsi
takwimu hizo zilivyopatikana na TBC iwaombe radhi Watanzania.
Alisema Mei 15, TBC ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho cha
Waislamu, Pazi Mwinyimvua na kuomba radhi kwa kasoro iliyotokea na
kueleza kwamba shirika lake limemwonya mfanyakazi aliyerusha hewani
takwimu hizo kimakosa.
“Nichukue fursa hii tena kuwaomba radhi ndugu zetu wa dini ya Kiislamu
kutokana na maumivu waliyopata kutokana na takwimu hizo. Na kwa kuwa
huu ni mwezi mtukufu wa Ramadhani na moja ya mahitaji wakati wa mfungo
ni kusameheana, naomba waumini wote wa dini ya Kiislamu wapokee kwa moyo
wa upendo ombi hili la kuwataka radhi,” alisema Mshana.
Aliongeza kwamba kwa kuwa suala hili limehusishwa na sensa ya watu na
makazi, anawaomba waumini wa dini ya Kiislamu kusamehe kilichotokea na
washiriki katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 26, mwaka
huu.
Wakati serikali ikiendelea kuhimiza wananchi kushiriki sensa, kuna kundi la Waislamu limejitokeza kupinga tukio hilo.
Walimu 108 waenguliwa kwenye semina ya Sensa Dar
Kundi hilo limekuwa likipita sehemu mbalimbali nchini kueneza sumu ya
kuwataka Waislamu wasishiriki sensa kwa madai kuwa serikali imelenga
kuwabagua kwa kutangaza takwimu zinazoonesha Wakristo ni wengi zaidi ya
Waislamu.
Mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Issa Sadick, hivi karibuni alizitaja
baadhi ya sababu za kukataa kuhesabiwa kuwa ni serikali kuendelea
kuwabagua Waislamu katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hata hivyo Sheikh Mkuu Mufti Shabaan bin Simba hivi karibuni aliwataka
Waislamu kushiriki sensa na walipuuze kundi la masheikh linalozunguka
nchini kutaka wasusie.
Wakati huo huo, walimu 108 walioteuliwa kuhudhuria semina ya makarani
wa sensa, wameenguliwa na nafasi zao kuzibwa na watu wengine.
Utafiti wa gazeti hili umebaini kuwa, walioenguliwa ni walimu wa Kituo cha Mafunzo cha Sekondari Tambaza jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa habari hizo, walimu hao wameenguliwa kutokana na kushindwa kufanya vizuri kwenye mtihani wa majaribio.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya walimu hao
walisema wanapinga kuondolewa kwao kwani walikwishakubaliana katika
mkataba wa malipo, na tayari walishaanza mafunzo kwa ajili ya kazi ya
ukarani wa sensa.
Walisema kuwa wahusika wamekuwa wakiwaleta ndugu zao na kuwapunguza walimu ambao tayari walishaanza mafunzo kwa siku nne sasa.
Walimu hao walisema wanaitaka serikali iwalipe fedha zao za siku nne ambazo tangu waanze mafunzo hayo hawajalipwa.
Taarifa hii imeandaliwa na Zawadi Chogogwe, Agness Newa na Stella Mushi wa Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment