ZAIDI ya watu 15, wakiwamo waandishi wa habari, jana
wamenusurika kifo baada ya magari matatu yaliyokuwa kwenye msafara wa
Mwenge wa Uhuru, kugongana wilayani Bunda, mkoani Mara.
Katika tukio hilo, magari mawili yameharibika vibaya, likiwamo la
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambalo ndani yake
walikuwamo waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, akiwamo mwandishi
wa habari hizi ambao walipata majeraha kiasi.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema chanzo cha ajali ni mwendo kasi,
ambapo gari moja mali ya halmasauri ya wilaya lenye namba za usajili SM
8809, lililigonga kwa nyuma gari la TAKUKURU lenye namba za usajili T
645 BCT.
Hali hiyo ilisababisha magari mengine likiwamo la TRA lenye namba za usajili
STJ 9663 kugongana na kuacha njia na
bila juhudi za madereva wa magari
mengine kufanya jitihada za makusudi
kwa kuacha barabara na kuingia upande mwingine huenda ajali hiyo ingesababisha madhara makubwa.
Polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa ajili hiyo na kusema
ilitokea majira ya jioni katika Kijiji cha Kasahunga, kwenye barabara
kuu ya Bunda-Ukerewe, wakati msafara huo wa Mwenge huo ukielekea kwenye
mkesha katika Kijiji cha Kibara, baada ya kuzindua na kuweka mawe ya
misingi kwenye miradi tisa ya maendeleo iliyogharimu zaidi ya sh
bilioni 1.4.
No comments:
Post a Comment