MHARIRI wa siku nyingi, Alfred Mbogora na Ofisa Habari wa Baraza
la Habari Tanzania (MCT), amefariki dunia jana alfajiri katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa jana kwa vyombo vya habari na
Katibu wa Jukwaa la Wahriri Tanzania (TEF), Neville Meena, marehemu
alilazwa katika hospitali hiyo kwa takriban siku tatu.
Taarifa hiyo ya TEF, ilibainisha kuwa Katibu Mtendaji wa MCT, Kajumbi
Mukajanga amesema Mbogora alilazwa Muhimbili tangu Agosti 14 baada ya
kuanguka katika eneo la Tegeta, mara baada ya kupata chakula wakiwa
njiani kwenda Bagamoyo kwa shughuli za kikazi.
Mukajanga alibainisha kuwa kabla ya kuanguka, Mbogora alikuwa
akilalamika kwamba anasikia kuishiwa nguvu kwenye mguu na mkono na
alipojaribu kusimama ili kutembea kutokana na hali aliyokuwa akiisikia
mwilini alianguka.
Tangu alipoanguka marehemu Mbogora alikata kauli na hakuweza kusema chochote hadi mauti yalipomfika jana alfajiri.
“Ni pigo kwa sekta ya habari nchini, kumpoteza mwanahabari mwenzetu
ambaye ametoa mchango mkubwa katika sekta yetu ya habari,” alisema.
Wakati huo huo, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa pole kwa
familia ya Mbogora, MCT na wanahabari wote nchini kutokana na kifo cha
mwanahabari huyo mkongwe.
No comments:
Post a Comment