WABUNGE wameibana serikali, wakiitaka iache ubabe wa kusitisha
mgogoro wa walimu kwa kutumia mahakama badala yake itafute ufumbuzi wa
kudumu kwa madai yao.
Wakati kambi rasmi ya upinzani bungeni ikisema kuwa hatua ya wabunge
kuzuiliwa kujadili mgogoro huo ni kitendo cha kulihujumu Bunge lenye
haki ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri serikali, Mbunge wa Kahama,
James Lembeli (CCM), alisema Tanzania ni nchi ya wafanyabiashara,
matapeli na wahuni kwa kuwa ndio wanaoweza kufanikisha mambo yao.
Akichangia mjadala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi jana,
Lembeli, alisema ametoa kauli hiyo kuwa walimu, madaktari na wakulima
kwa miaka mingi wamekuwa wakilalamika bila kutatuliwa matatizo yao.
Alisema kuwa wakati wa kuficha mambo umekwisha na kuhoji iwapo serikali haioni matatizo ya walimu, madaktari na wakulima.
“Nikimaliza Bunge naenda jimboni. Mimi nadai posho kila siku, mbona
sijapelekwa mahakahamani? Kama fedha haipo waambiwe na iwe kwa wote si
wachache waendelee kuneemeka. Nchi hii ni ya wafanyabiashara, matapeli
wahuni kwa sababu ndio wanaweza kufanikisha mambo yao.
“Serikali inasema madaktari wamerudi kazini, lakini hawafanyi kazi.
Mimi nimezungumza haya kwa sababu nasema ukweli na msema kweli mpenzi wa
Mungu. Ukweli ndio huo na ukweli unauna, walimu tuwahurumie, wao ndio
waliotuchagua kuja bungeni. Waziri atakapokuwa akihitimisha nataka
nimsikie aseme hii ni ya watu gani,” alisema.
Pamoja na hayo, alilaani kitendo cha serikali kukimbilia mahakamani
kuzima mgomo wa walimu na kusema walimu hawahitaji kubezwa.
“Hii ni sawa na baba na mama wanagombana na kisha baba anakimbilia
polisi… walimu wamerudi kazini, lakini hawafanyi kazi. Mshahara wa sh
200,000 mwalimu ataishije? Kama sisi wabunge tunalalamika kwa nini
tusiwatetee? Kuna haja ya serikali kuzungumza na walimu, madaktari,
wakulima,” alisema.
Naye Susan Lyimo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani alisema kuwa
kutokuwapo kwa mgomo halisi kusiifanye serikali ifikiri kwamba imemaliza
tatizo la madai ya walimu, kwani kuna migomo baridi ambayo athari zake
huwa mbaya zaidi ya migomo halisi.
Alibainisha kuwa iwapo walimu wataachwa na kinyongo kama walivyo sasa,
na kama wataamua kulipa kisasi kwa kuwafundisha watoto vitu visivyo
halisi, kuna hatari kubwa kuwa na kizazi kisicho na elimu kabisa na
hatimaye kuwa na taifa lisilojiweza katika nyanja zote.
Kutokana na hali hiyo, kambi hiyo imeishauri serikali kufanya
mazungumzo na Chama cha Walimu nchini (CWT), ili kufikia maridhiano na
hivyo kusonga mbele katika kuboresha elimu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Maulida Komu (CHADEMA)
akichangia hoja hiyo, alikemea tabia ya serikali kumbilia mahakamani
kuzima migomo pamoja na kushindwa kuchukua juhudi za dhati kuboresha
sekta ya elimu nchini.
“Tunajenga taifa la aina gani? Watoto wanatoa vibiyongo kwa kukaa
chini, halafu ninyi bado mnacheka cheka…ndio nchi hii itachukuliwa.
Kwani vita maana yake nini? Yote yatatokana na wananchi kuchoka.
“Tuzingatie elimu, tutafakari ni kitu gani kifanyike kuikomboa elimu yetu na si kuendelea kucheka cheka,” alisema.
Akizungumzia wanafunzi wanaomaliza darasa la saba huku wakiwa hawajui
kusoma na kuandika, msemaji wa kambi ya upinzani, alimtaka Waziri wa
wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Phillipo Mulugo,
kuwajibika kutokana na sakata hilo.
Pamoja na hilo, aliitaka serikali kutoa tamko rasmi bungeni kuhusiana
na jambo hilo, ili jamii iweze kuelewa kinachochangia hali hiyo.
“Kambi ya upinzani inashangaa mpaka sasa Waziri wa Elimu na Naibu wake
bado wapo madarakani wakishangilia ushindi wa kuliongoza taifa kushika
nafasi ya kwanza duniani kufaulisha wanafunzi 5,200 wasiojua kusoma na
kuandika,” alisema Lyimo.
Mbunge wa Mbozi, Godfrey Zambi, aliitaka serikali kuwachukulia hatua
walimu na wasimamizi wa mitihani ambao watabainika kuwapatia mitihani
wanafunzi.
Alisema watumishi wa serikali wakiwamo walimu wanagoma kutokana na
maslahi duni na kueleza kuwa kuna haja kwa serikali kulizingatia suala
hilo.
“Walimu wanafanya kazi kubwa na ngumu… wote tuliomo humu ndani
tunatokana na walimu, hivyo kuna ulazima wa serikali kuzingatia matatizo
ya walimu. Kuvutana, kupelekana mahakamani hakutatusaidia,” alisema.
Akisoma taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii,
Martha Mlata, alisema kamati imebaini utaratibu unaotumika kutoa mikopo
ya elimu ya juu haukidhi mahitaji ya wanafunzi hususan wanaotoka katika
familia duni.
Mlata alisema kamati inasikitishwa na hali ya kukosa masomo kwa
baadhi ya wanafunzi wanaojihusishana na vitendo vya migomo katika
taasisi mbalimbali nchini ikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam na IMTU.
Awali, akiwasilisha bajeti yake, Waziri Kawambwa, alisema katika mwaka
huu wa fedha, wizara kupitia Bodi ya Mikopo itatoa mikopo kwa wanafunzi
98,772 wa vyuo vya elimu ya juu.
Alisema pamoja na hilo, itasimamia ukusanyaji wa marejesho ya mikopo
ya sh bilioni 18 kwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wadaiwa na
waaajiri watakaoshindwa kutimiza wajibu wao na kuwatafuta wadaiwa
kupitia viongozi wa serikali za mitaa.
Alisema mwaka jana, wizara ilitoa mikopo kwa ajili ya chakula, malazi,
vitabu na viandikia kwa wanafunzi 93,176 wakiwamo wahadhiri 256.
Dk. Kawamba aliliomba Bunge kuridhia mapato na matumizi ya sh bilioni 724.471 kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
No comments:
Post a Comment