Na Mwandishi Wetu kutoka gazeti la Majira
SIKU chache baada ya kutokea mauaji yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa dhidi ya mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, habari zilizolifikia gazeti hili zinasema Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, yupo mbioni kuhamishiwa Makau Makuu.Vyanzo mbalimbali vya kuaminika ndani ya jeshi hilo vilidai kuwa, Kamanda Kamuhanda atahamishiwa Makao Makuu, Dar es Salaam, lakini haijajulikana atapangiwa kazi gani.
Inaelezwa kuwa, uhamisho huo utafanyika mara moja baada ya kamati iliyoundwa na Waziri wa Mamno ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kumaliza uchunguzi wa mazingira ya kifo cha marehemu Mwangosi anayedaiwa kupigwa bomu.“Wakubwa wetu wamepima na kupitia rekodi ya utendaji wa Kamuhanda, hatua za awali atalazimika kuhamishiwa Makao Makuu, Dar es Salaam.
“Kutokana na mazingira ya kifo cha Mwangosi ni wazi Kamuhanda hawezi kuendelea na kazi mkoani Iringa, pamoja na mashinikizo mbalimbali yanayotolewa na wanahabari kutaka awajibishe,” kilisema chanzo hicho na kusisitiza kuwa;“Sababu nyingine ya kuhamishwa Makao Makuu ni mauaji yaliyotokea kwenye mikoa aliyokaa, alipokua mkoani Ruvuma watu wanne walipoteza maisha mjini Songea wakati wa maandamano,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Bi. Advera Senso, alipoulizwa kuhusu ukweli wa taarifa hizo, alisema; “Taarifa hizo sina, kama zingekuwepo ningewaambia”.Aliongeza kuwa, kama uhamisho huo utakuwa wa kweli ni utaratibu wa kawaida kwa makamanda kuhamishwa vituo vya kazi na kupelekwa sehemu zingine.Hivi karibuni, Jeshi la Polisi mkoani Iringa linadaiwa kufanya mauaji ya Mwangosi katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi, wakati viongozi wa CHADEMA, wakifungua matawi na kufanya mikutano ya ndani.
Baada ya kutokea mauaji hayo, Kamanda Kamuhanda alisema polisi walilazimika kutumia nguvu ya ziada kutokana na wananchi kukaidi amri halali ya kuwataka watawanyike.
No comments:
Post a Comment