SIKU chache baada ya klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kutangaza kumfukuza kocha wake Mbelgiji, Thom Saintfiet, aliyekuwa kocha wake wa zamani, Mserbia Kostadin Papic ameibukia Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), akiishtaki kwa kushindwa kumlipa stahiki zake za kusitisha mkataba wake.
Mserbia Kostadin Papic.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, alisema Yanga wanatakiwa kutoa ufafanuzi haraka juu ya madai ya Papic, kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa kutokana na mashitaka yanayowakabili kuwa mazito.
Alisema kuwa walipokea barua kutoka FIFA, ambayo imeelezea kutimuliwa kwa Papic, pasipo kulipwa malimbikizo ya mshahara, dola 12,300 za Marekani, jambo ambalo alibainisha ni aibu kwa klabu hiyo na taifa kwa ujumla.
“Yanga wanatakiwa watumie misingi sahihi ya kuwaondoa makocha wake badala ya kutumia njia zisizofaa, hali ambayo inaiweka klabu hiyo katika mazingira ya kutoaminiwa na makocha wa kigeni na kutudhalilisha sisi,” alisema Osiah.
Akizungumzia suala la kutimuliwa kwa Saintfiet, Osiah alisema kuwa TFF wamehuzunishwa na hatua hiyo, licha ya kuwa shirikisho hilo bado halijapewa barua rasmi.
Pia Osiah alisema kutimuliwa kwa sekretarieti yote ya Yanga ni uonevu, kwa kuwa hawakutendewa haki.
“Tunasikitika sana, kwa kuwa wote waliotimuliwa hawajatendewa haki, kwa kuwa sisi wenyewe kama TFF tunawatumia wao katika kufanya kazi zetu, kwa kuwa mara kwa mara tunawapa semina za kiuongozi ili kuwawezesha kufanya kazi inavyotakiwa, hivyo kuondolewa kwao ni hasara kwetu pia,” alisema Osiah.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Yanga kufuata kanuni na taratibu ili kuondoa migogoro mbalimbali inayojitokeza mara kwa mara katika klabu hiyo, kwa kuwa inapoteza sifa kwa mashabiki na wapenzi wake, kwa kuporomosha kiwango cha utendaji.
No comments:
Post a Comment