Jeshi la Polisi wilayani Ukerewe mkoani Mwanza limewafikisha mahakamani walimu watano kwa tuhuma za wizi wa mtihani wa Taifa wa darasa la saba huku mwalimu mwingine aliyetoroka akiendelea kusakwa.Walimu hao walifikishwa katika Mahakama ya wilaya hiyo juzi na kusomewa mashitaka mbele ya mlinzi wa amani, Charles Bilomela, ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.
Walimu hao ni pamoja na aliyekuwa msimamiazi wa mtihani wa Taifa wa darasa la saba mkondo C katika shule ya msingi Hamkoko, Leonida Anthony (32), ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Busumba.Washitakiwa wengine ni walimu wa Shule ya Msingi Hamkoko Kija Songoli (30), Jenifreda Edward (28), Mariam Kateti (26) na Marycelina Marcel (25).
Mwalimu mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Diana Shishanga anayetuhumiwa kushiriki kutenda makosa hayo anatafutwa na polisi ili aunganishwe na wenzake katika kesi hiyo.Mwendesha mashitaka wa Polisi, Inspekta Samwel Onyango, alidai kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo Septemba 19, mwaka huu saa 5:10 asubuhi katika Shule ya Msingi Hamkoko.
Alidai kuwa wanakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kula njama na kutenda wakiwa watumishi wa umma.Kosa la pili ni wizi wa mtihani wa Taifa wa darasa la saba na kupatikana na nyaraka za serikali ambazo ni mali ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kinyume cha sheria kifungu cha 183 cha makosa ya jinai.
Alidai washitakiwa walikamatwa nyumbani kwa mwalimu Kija Songoli wakiandaa majibu ya mtihani wa Hisabati kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi majibu ya mtihani huo.Walimu hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa hakimu mwenye mamlaka ya kusikiliza kesi zinazofikishwa katika mahakama hiyo, Rouben Luhasha, yupo nje ya wilaya kikazi.
Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 8, mwaka huu na watuhumiwa wapo nje kwa dhamana yenye masharti kadhaa likiwemo la kufika katika mahakamani hapo kila Ijumaa huku wakizuiwa kutoka nje ya Wilaya bila kibali cha Mahakama.
No comments:
Post a Comment