MWANAFUNZI wa kidato cha sita aliyefaulu kujiunga na Chuo cha Ualimu Marangu mkoani Kilimanjaro, Debora Kenogo (20) amemfikisha mahakamani baba yake mzazi ili amlipie ada baada ya kugoma akitaka aolewe.
Debora amemshitaki baba huyo, Zablon Kenogo ambaye ni mfanyabiashara mjini hapa, katika Mahakama ya Mwanzo, baada ya kugoma kumlipia ada ya Shilingi 600,000.
Shauri lake limefunguliwa kwa namba 132/2012 na limeanza kusikilizwa. Awali, binti huyo ambaye anatakiwa kujiunga na Chuo cha Marangu kwa masomo ya Stashahada ya Ualimu, alimshitaki baba yake katika ofisi za Idara ya Ustawi wa Jamii, na kufungua malalamiko. Baba yake aliitwa, lakini aligoma kumlipia ada hiyo binti huyo aliyefaulu masomo yake. Septemba 12, ofisi ya Ustawi wa Jamii ya Wilaya iliandika barua kwenda Mahakama ya Mwanzo Tarime ikaipokea na kufungua kesi ya madai namba 132/2012.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mwandamizi Jarome Migera huku binti huyo akidai kuwa baba yake amegoma kumlipia ada ya chuo na kwamba anataka aolewe, jambo ambalo binti huyo amegoma na anaomba msaada ili amalizie masomo yake, badala ya kukatishwa kwa tamaa ya baba kujipatia mahari.
Kesi hiyo imevuta mamia ya watu mjini hapa kutokana na wazazi wengi kuwa na tabia ya kufikiria kuoza binti zao badala ya kugharimia masomo.
via HabariLeo
No comments:
Post a Comment