MWANAFUNZI wa kidato cha nne katika Sekondari ya Alfa Germ, Morogoro, Jessica Kiliani (17), amelazimika kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu hiyo akiwa wodini baada ya kufanyiwa upasuaji.
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Alfa iliyopo Manispaa ya Morogoro, Jesca Kiliani akifanya mtihani wa taifa wa kidato hicho akiwa wodini katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani Morogoro, jana, alikolazwa kwa ajili ya matibabu baada ya kufanyiwa oparesheni. Wanafunzi wa kidato cha nne nchini waameanza mitihani ya kuitimu kidato hicho. Picha na Juma Mtanda.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mwanafunzi huyo, kuomba aruhusiwe kufanya mtihani huo licha ya kuwa wodini akiugulia maumivu ya upasuaji aliofanyiwa na madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa zaidi saa ya mbili na kulazwa katika wodi ya wazazi namba 7B.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Anna Ngapemba alisema alipigiwa simu na mkuu wa shule hiyo 6:00 usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili iliyopita akimjulisha kuwa binti yake anasumbuliwa na tumbo na anahitaji msaada wa haraka.
Ngapemba alisema alilazimika kwenda shuleni hapo usiku huohuo na kukutana na mama mlezi (matron) wa hosteli za shule hiyo na kujulishwa juu ya hali ya binti yake na kwa kushirikiana na uongozi wa shule hiyo, walimpeleka katika Hospitali ya Mkoa.
Alisema wauguzi waliokuwa zamu usiku huo walilazimika kumpigia simu daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Christopher Manumbu ambaye alifika na kumfanyia upasuaji kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Mama huyo alisema binti yake aliwahi kulalamika kuwa na maumivu ya tumbo akiwa kidato cha pili mwaka 2010 lakini baada ya kupatiwa matibabu, hali hiyo haikumtokea tena hadi Jumamosi iliyopita.
Baada ya upasuaji huo, Dk Manumbu alisema binti huyo alihitaji upasuaji wa haraka ili kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Akiwa chini ya msimamizi wa mitihani na polisi, Jessica licha ya kuwa katika hali ya maumivu alifanya mitihani miwili kama wenzake wa kidato hicho. Mitihani hiyo ni Uraia na Kiingereza.
Mwanafunzi huyo alisema hakuwa tayari kuikosa mitihani hiyo na ndiyo maana alimwomba mama yake kuwasiliana na uongozi wa shule yake ili umwandalie mazingira mazuri ya kufanya mtihani akiwa wodini.
Alifanya mitihani yote miwili akiwa katika Wodi ya Wazazi namba 7B, katika chumba cha pekee.
Watahiniwa Jitegemee chupuchupu
Zaidi ya wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari Jitegemee, Dar es Salaam nusura wasifanye mtihani wao wa kidato cha nne kutokana na kutokuwa na vitambulisho vinavyowaruhusu kuingia katika chumba cha mtihani.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Luteni Kanali Martin Mkisi alisema jana kuwa wanafunzi hao walisahau vitambulisho hivyo lakini waliombewa kwa msimamizi mkuu wa mitihani hiyo.
“Changamoto huwa hazikosekani licha ya kuwaandaa vizuri wanafunzi, lakini wamesahau vitambulisho, kama mkuu wa shule nilichukua jitihada ya kuwaandikia ujumbe mfupi wa utambulisho ili waweze kufanya mtihani,” alisema Mkisi.
Akizungumzia mtihani huo, mmoja wa watahiniwa katika shule hiyo, Hafsa Ramadhani alisema ulikuwa mzuri kutokana na maandalizi aliyofanya.
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Tanzania Bara ulianza jana na unatarajiwa kumalizika Oktoba 25, mwaka huu.
Habari hii imeandikwa na Venance George na Juma Mtanda, Morogoro; Magreth Munisi, Deborah Ngajilo na Aisha Ngoma
No comments:
Post a Comment