RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, itakayofanyika kitaifa mkoani Shinyanga.
Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mkangara, alisema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Oktoba 14.
“Wote tunafahamu Oktoba 14 ya kila mwaka Watanzania tunaadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, hivyo serikali pia imeamua kuunganisha maadhimisho hayo na sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana Kitaifa,” alisema Mkangara.
Alisema falsafa ya mbio za Mwenge wa Uhuru ni kuwashirikisha zaidi wananchi kuutumia mwenge kutunza na kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa kitaifa na kuhimiza maendeleo ya wananchi bila kujali itikadi za kisiasa, dini na ukabila.
“Pamoja na malengo ya jumla ya kuanzisha wiki ya vijana mwaka 2000, shughuli hizo mwaka huu zitajielekeza zaidi katika kuhamasisha juhudi na mikakati ya serikali katika kuwawezesha vijana kujitambua, kujitolea, kujitegemea na kuthubutu kwa malengo chanya ya kujiajili na kuajili vijana wengine,” alisema Mkangara.Habari na Hosea Joseph
No comments:
Post a Comment