Madiwani wa Halmashauri Wilaya ya Singida wamekana kumwandikia barua Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri, inayomkataa mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa wakuu wa wilaya Singida na Ikungi, inaeleza kuwa madiwani hao hawana imani na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Illuminata Mwenda.
Katika Kikao cha Baraza la Madiwani lililokutana juzi mjini Singida, walisema wanashangazwa na maelezo yaliyopo kwenye barua hiyo, wakidai kuwa labda imeandikwa na mtu mmoja kwa nia ya kuwagonganisha na watendaji wa halmashauri hiyo.
Baadhi ya madai ya barua hiyo iliyosomwa mbele yao na mkuu wa wilaya Ikungi, Manju Msambya ni Mkurugenzi mtendaji kupuuza maamuzi mbali mbali ya madiwani inapofikia wakati wa kuwafukuza watumishi wabovu.
Madai mengine ni kugoma kuwahamisha watumishi waliotumika katika halmashauri hiyo kwa zaidi ya miaka kumi, kuigeuza halmashauri shamba la bibi na kukumbatia watumishi wabadhirifu idara ya fedha na Afya.
Baada ya barua hiyo iliyotumwa kwa Naibu waziri na nakala kupewa wakuu hao wa wilaya, Ikulu, Waziri Mkuu, Mkuu wa mkoa na wabunge wa Singida, kusomwa, mwenyekiti wa Halmashauri Celestine Yunde aliomba aliyeiandika barua hiyo ajitokeze kutetea hoja zake, lakini hata hivyo hakuna aliyethubutu kusimama.
“Waheshimiwa madiwani, kila mmoja amesikia barua hii ilivyosomwa, naomba aliyeandika asimame ili atetee hoja hii, nadhani yupo miongoni mwetu,"aliwauliza madiwani waliohudhuria baraza hilo bila kupata jibu.
Hata hivyo madiwani mbali mbali walijitokeza kulaani kitendo hicho, kwa madai kuwa aliyeandika barua hiyo hakuwa na nia njema kwa wilaya hiyo.
Aidha baraza hilo kwa pamoja lilikubaliana kuchunguza kwa undani sakata hilo, ili aliyehusika achukuliwe hatua za kinidhamu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment