MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, amezungumzia mustakabali wake huku akisisitiza kuwa kamwe hajafungwa mdomo bali anajipanga kuanika ukweli wa kile kilichomsibu.
Dk. Ulimboka ambaye alitekwa, kuteswa, kuumizwa vibaya na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaamu usiku wa kuamkia Juni 27 mwaka huu, amekuwa kimya baada ya kurejea nchini akitokea Afrika Kusini alikokwenda kwa matibabu zaidi.Tangu kurejea nchini mapema Agosti, Dk. Ulimboka amekuwa mafichoni kutokana na kile kilichoelezwa ni kutotaka wabaya wake wajue alipo ili wasijewakamdhuru na kupoteza ushahidi hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa akiwataja hadharani baadhi ya maofisa wa Usalama wa Taifa akidai walishiriki kumteka.
Hata hivyo, ukimya wake umeibua mjadala kiasi cha watu wengine kuanza kudhani kuwa amenyamazishwa asisema chochote juu ya tukio hilo ambalo limelighubika taifa kutokana na mkanganyiko uliyopo.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana baada ya ukimya huo, Dk. Ulimboka alisema kamwe hawezi kuzibwa mdomo kama ambavyo taarifa za uvumi zilivyozagaa. Alisema kuwa muda ukifika atazungumzia masuala yote yanayohusiana na kutekwa kwake na hatua gani zitakazofuata, “Siwezi kuzibwa mdomo na yeyote, hata walionichagua kuwa mwenyekiti wao, wanafahamu hivyo, suala ni wakati tu, utakapofika hasa baada ya kukamilisha masuala ya kisheria, nitazungumza hivi karibuni ili kuondoa hofu hiyo,” alisema.
Dk. Ulimboka pia amewataka wanataaluma wenzake kutulia hasa kwa wakati huu ambao bado ameweka kipaumbele katika tiba yake ambayo ameielezea kuendelea kuimarika na kwamba madai yao bado ni ya msingi na kamwe hayawezi kuishia hapo yaliposimamia.
No comments:
Post a Comment