Habari na Hillary Shoo, Manyoni.
WANANCHI wa kijiji cha Mwanzi, wameilalamikia Hospitali ya
Wilaya ya Manyoni kutokana na kitendo cha kuwatoza fedha na vitenge
kinamama wajawazito wanapokwenda kujifungua.
Wakazi hao walitoa kilio hicho kwenye kikao maalumu kati yao na timu
ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii waliotembelea
kijiji hicho kujua utekelezaji wa mradi wa ushiriki sawa wa wanaume
katika masuala ya afya ya uzazi na jinsia.
“Bora na nyie mmekuja ili nasi tuweze kutoa kilio chetu, ni ukweli
usiopingika kwamba unapofika hospitali muuguzi anakuambia kama huna hela
utaipata, maana hatukuhudumii, we kaa hapo ukisubiri huduma ya bure.
Hapa hakuna huduma ya bure,” alisema Zainabu Juma.
Alisema wamekuwa wakitozwa kati ya sh 20,000 na 30,000, ili kuweza
kupatiwa huduma ya kujifungua na wakati mwingine wanaambiwa waende na
vitenge 20.
“Hivi kweli jamani vitenge 20 vya nini, mimi najua kuwa huduma kwa
kinamama wajawazito zinatolewa bure, lakini hapa Manyoni hilo halipo,”
alilalamika.
Akijibu malalamiko hayo, Dk. Mapela alisema ni makosa kumtoza mama mjamzito fedha, kwani huduma hizo zinatolewa bure.
Kwa upande wake, muuguzi kutoka Hospitali ya Manyoni, aliwataka
kinamama hao kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa
wahusika, ikibidi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
ili wanaofanya mchezo huo wawajibishwe.
No comments:
Post a Comment