Idadi kubwa ya wafungwa wanaomaliza muda wa kutumikia vifungo vyao
katika magereza mbalimbali nchini wanashindwa kukaa uraiani badala yake
wanafanya mbinu za kurejea kwenye magereza.
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Dk. Immanuel Nchimbi |
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya ndani
ya Nchi, Dk. Immanuel Nchimbi wakati akizindua karakara ya kutengezea
magari pamoja na namba mpya za magari katika Gereza la Ukonga jijini Dar
es Salaam jana.
Alisema katika utafiti imebainika kati wa
wafungwa 100 wanaomaliza muda wao wa kifungo, 35 wanarudi tena gerezani
baada ya kufanya vitendo vya kihalifu kwa makusudi .
Dk. Nchimbi alisema sababu kubwa
inayosababisha kukithiri kwa hali hiyo ni tatizo la Jeshi la Magereza
kutoweka kipaumbele kuwarekebisha kwa kuwapa mafunzo mbalimbali ya
ufundi ili wanaporejea uraiani wawe kazi ya kufanya.
"Wimbi la watu wanaomaliza kifungo chao na
kurejea tena gerezani linazidi kukua, kibaya zaidi watu hawa wanafanya
makosa kwa makusudi wakijua watafungwa gerezani baada ya kushindwa
kuishi kutokana na kutokuwa na kitu cha kufanya," alisema Dk. Nchimbi.
Hata hivyo, alisema uanzishwaji wa
karakara ya magari ndani ya Gereza hilo utatoa nafasi kwa wafungwa
kujifunza ufundi na watakapomaliza kifungo wataendeleza kazi hiyo.
Hata hivyo, Dk. Nchimbi alisema mradi huo
wa utengenezaji wa magari uonyeshe mwanga wa utumishi bora wa Jeshi kwa
magari yanayopelekwa hapo na taasisi mbalimbali za Serikali yatengenezwe
kwa muda unaokubalika na gharama nafuu.
Alisema imekuwa kawaida kwa miradi mingi
ya Serikali kuwa na nguvu ya soda kwa kufunguliwa kwa mbwembwe kubwa,
lakini inapoanza kazi haidumu kwa siku nyingi na kuzusha malalamiko kwa
wateja.
"Nimeona hapa mradi huu tunauzindua kwa
mbwembwe lakini sitegemei ndani ya mezi sita mambo yanakuwa mabaya,
imani yangu mtazidi kutuonyesha kuwa miradi yote inayoanziushwa na Jeshi
inakuwa bora," aliongeza kusema.
Waziri Dkt. Nchimbi alisema kuna haja kwa
sheria ya manunuzi ya Serikali kuangalia upya kwani nyingi haziendi na
wakati na kusababisha ukwamaji wa vitu mbalimbali.
Akizungumzia namba mpya za magari za
Magereza zinazoanzia na maneno ya MT, Waziri huyo alisema uamuzi huo
unalenga kulitambulisha rasmi na kuweka uwazi kwa wananchi wote.
Awali kamishna Mkuu wa Magereza, John
Minja alisema kuanzishwa kwa karakana hiyo kutaongeza kasi ya utendaji
kazi kwa askari kurekebisha wafungwa kwa vitendo pamoja na kurahisisha
jeshi hilo pamoja na Taasisi za Serikali kutumia pesa nyingi kutengeneza
magari kwa taasisi zingine.
Aidha alisema namba za magari zimeanza
kutumika baada ya waziri husika kuridhia kifungu namba 114 sura 168 ya
usalama barabarani kama alivyopewa jukumu hilo kisheria.
No comments:
Post a Comment