Serikali
imeamua kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya wanafunzi na walimu
katika shule ya Sekondari Bagamoyo mkoa wa Pwani kufuatia mgogoro
uliotokea na kusababisha shule hiyo kufungwa Novemba 5, mwaka huu.
Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Mafunzo ya
Ufundi, Eustella Bhalalusesa akisoma ripoti ya uchunguzi jana jijini Dar
es Salaam kwa niaba ya waziri, Dk Shukuru Kawambwa alisema wanafunzi
waliothibitika kuwa vinara wa vurugu bila kutaja idadi yake
watachukuliwa hatua za kinidamu ambazo hakuzieleza.
Pia alisema walimu walioonekana kutowajibika ipasavyo nao watachukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.
Alisema shule hiyo ilifungwa siku hiyo
baada ya kuwepo kwa dalili za kuvunjika kwa amani na utulivu kitendo
ambacho wizara yake iliamua kuunda kamati kuchunguza chanzo cha mgogoro.
Dk Kawambwa alisema uchunguzi umebaini
kuwa, chanzo kikuu cha mgogoro huo ni mfarakano kati ya uongozi wa shule
na baadhi ya wanafunzi ambapo kulitokea kutoelewana na mabadiliko ya
kinidhamu yaliyotangazwa shuleni hapo.
Pia alisema mkuu huyo wa shule aliwataka
wanafunzi watie mkazo katika masomo yao kitendo ambacho baadhi ya
wanafunzi walikipinga na kusababisha kuwepo kwa mgogoro huo.
Alisema kamati hiyo imegundua kuwa
kukosekana kwa umoja wa kikazi miongoni mwa walimu, utoro wa walimu
kazini na utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi kumechangia kwa kiasi
kikubwa kukua kwa mgogoro huo.
Alisema serikali imeamua, ili kutoa nafasi
kwa uongozi wa shule kujipanga upya, wanafunzi wote waliothibitika
kutoshiriki katika mgomo watarudi shuleni mwezi Januari mwakani kwa
utaratibu utakaowekwa.
Alisema kwa wanafunzi wa kidato cha sita
ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwezi Februari mwakani, upo
utaratibu unaofanywa ili kuwezesha walimu wao kuwafundisha maeneo ambayo
watakuwa hawajasoma.
Pia serikali imewaagiza wakuu wote wa
shule nchini kuchukua hatua za haraka na watoe taarifa kwa viongozi wa
Halmashauri za Wilaya na Mikoa pindi wanapogundua dalili za mgogoro ili
hatua zichukuliwe.
Alisema wanafunzi wanapaswa kufuata njia halali kufuatilia mahitaji yao.
Kuhusu suala la udini kama lilivyotajwa
awali kuwa ni sehemu ya mgogoro huo. Bhalalusesa alisema wizara yake
haiwezi kukataa au kukubali kwa sababu ndani ya shule hiyo kulikuwa na
uhuru na utovu wa nidhamu uliopitiliza hadi ilifikia mwaka jana mmoja wa
walimu shuleni hapo kubakwa.
Kuhusu utoro wa walimu, Bhalalusesa alisema baadhi yao wanakaa Dar es Salaam hivyo hutumia kama kisingizio.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment