SIKU moja baada ya Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, kuibana
serikali akiitaka ifafanue juu ya upotevu wa sh bilioni 86 za kununulia
mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme, Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, amekwepa kuzungumzia suala hilo.
Wakati Waziri Muhongo akikwepa, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim
Maswi, na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Jenerali mstaafu
Robert Mboma, nao walishindwa kutoa ufafanuzi.
Katika taarifa yake juzi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma
Kaskazini (CHADEMA), akinukuu taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) iliyobaini upotevu wa mabilioni hayo pamoja na
mambo mengine alimtaka Waziri Muhogo aeleze hatua alizochukua baada ya
kukabidhiwa taarifa hiyo kuhusu maofisa waandamizi wa wizara waliohusika
na wizi huo.
Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, Waziri Muhongo, alipotafutwa
kwa njia ya simu ili azungumzie juu ya upotevu huo wa mabilioni ya
shilingi, alisema hana cha kujibu na kwamba taarifa hizo yeye
hajazisoma.
Alipotakiwa kuelezea hatua alizozichukua yeye kama waziri dhidi ya
wizi huo, Prof. Muhongo, hakuwa tayari bali alisema yeye sio mtu wa
kulumbana na kwamba kama kuna fedha zimeibiwa kuna taratibu za serikali.
“Tuongee mambo ya maendeleo, kuna wengine kulumbana ni kazi yao; sisi wengine taaluma zetu sio hizo,” alisema Prof. Muhongo.
Mapema gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, kuzungumzia taarifa hizo bila mafanikio.
Zitto katika taarifa yake mbali na Wizara ya Nishati na Madini pia
alimtaka Waziri wa Fedha na Uchumi aueleze umma juu ya kiwango cha fedha
ambacho Hazina imetoa kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme wa
dharura kati ya Novemba 2011 na Oktoba 2012.
Alipotafutwa, Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kuzungumzia juu ya
suala hilo, simu yake iliita bila kupokelewa na hata alivyotumiwa ujumbe
mfupi wa maandishi pia hakujibu.
Juzi, Zitto alibainisha juu ya kuwapo kwa ripoti zinazoonyesha kuwa
kuna kikundi ambacho kazi yake kubwa ni kujifaidisha binafsi na mpango
wa umeme wa dharura kupitia kwenye ununuzi wa mafuta mazito ya mitambo
ya IPTL.
Alisema juhudi zilizofanywa na Kamati ya Bunge ya Hezabu za Mashirika
ya Umma ambayo yeye ndiye Mwenyekiti wake, Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini, John Mnyika, na aliyekuwa Mwenyekiti wa Nishati na Madini,
January Makamba, za kutaka uchunguzi juu ya suala hilo ufanywe,
hazikuzaa matunda.
Katika kutafuta kiini cha upotevu, kwa mara nyingine, wa mabilioni ya
shilingi TANESCO, gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi hiyo,
Jenerali mstaafu Robert Mboma, bila mafanikio.
Hata hivyo, alipopigiwa Makamu Mwenyekiti wake, Victor Mambalaswa,
alisema yuko jimboni na kwamba taarifa hiyo ya CAG kuhusu upotevu wa
mabilioni hayo haijafika TANESCO.
“Kama kuna mtu kaiona hiyo taarifa itakuwa serikalini lakini TANESCO bado haijafika,” alisema Mwambalaswa.
Kwa upande wake Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, Mnyika, alisema
anaungana na Zitto kuwataka viongozi hao wa serikali watoe kauli kwa
umma akiwamo CAG na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).
Alisema iwapo kauli hazitatolewa kwa wakati atatoa nyaraka na majina ya wahusika.
Mnyika alisema alichoeleza CAG kwenye taarifa yake kama
ilivyonukuliwa kwenye gazeti la The East African la Novemba 24-30
kuhusu dola milioni 54 (bil. 86) ni sehemu tu ya tuhuma za ufisadi
zinazotokana na ukiukwaji wa sheria ikiwemo ya ununuzi katika
utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.Via Tanzania Daima.
“Lakini ukweli kuwa tuhuma za ufisadi, Waziri Muhongo, Waziri Mgimwa
na Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Jenerali Mbona wanapaswa kutoa kauli
kurejea taarifa ya Zitto ya jana na taarifa yangu ya Novemba 23 mwaka
huu,” alisema Mnyika.
No comments:
Post a Comment